Thursday, December 18, 2014

TIMU YA COSMO YA KIROMBA YATAWAZWA KUWA BINGWA JIMBO CUP MTWARA VIJINI BAADA YA KUIBANJUA TIMU NGUMU YA SUPER EAGLE YA MGAO.
Timu ya Cosmo ya Kiromba ikisherehekea ushindi wao wa jimbo cup
Michuano ya ligi jimbo cup Mtwara vijijini imehitimishwa juma tano ya tarehe 17/12/2014 kwa timu ya Casmo ya Kiromba kuigagadua timu ya Super Eagle ya mgao kwa mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa katika uwanja wa shule ya Msingi Nanguruwe Mtwara Vijijini.

Pamoja na timu ya Super Eagle kushinda mechi zote za awali za ligi hiyo, lakini walikuja kugonga mwamba mechi ya fainali na kukubali kichapo hicho toka kwa Cosmo na kutimia usemi usemao "Mpira Unadunda".

Mgeni rasmi katika fainali hiyo alikuwa na naibu waziri wa TAMISEMI Kassim Majaliwa akimwakilisha waziri wa TMISEMI Hawa Abrahamani Ghasia mbunge wa Mtwara vijijini ambaye pia ni mdhamini wa michuano hiyo.
Majaliwa aliwashauri viongozi wa chama cha soka mkoani mtwara MTWAREFA kupitia mwenyekiti wake Athumani Kambi kuviendeleza vipaji vilivyopatikana katika michuano hiyo, kwa kuwapeleka timu ya Ndanda B, ili kuondokana na kasumba ya kusajili wachezaji kutoka nje ya Mtwara.
Mshindi wa kwanza katika mashindano hayo timu ya Cosmo ya Kiromba amezawadiwa kitita cha shilingi 1,000,000 kikombe na seti ya jezi.
Mshindi wa pili Super Eagle ya Mgao imeibuka na kitita cha shilingi 700,000 na seti ya jezi.
Mshindi wa tatu Small Boys ya Dihimba  shilingi 500,000 na seti moja jezi.
Mshindi wa nne ni Nanyamba Kids ya Nanyamba ambao wamejinyakulia shilingi 300,000 na seti ya jezi.
Aidha  Saidi Nakaja wa Cosmo aliibuka kuwa  mchezaji bora, na nafasi mfungaji bora ilikwenda kwa Ally Mkisiwa wa Super Eagle aliyefunga magoli 11, wakati golikipa bora ni Haji Domanga kutoka Cosmo kila mmoja aliweza kupata seti moja ya jezi na nafasi ya mwamuzi bora ilikwenda kwa Jabiri Narumanga ambaye alizawadiwa shilingi 50,000.

Ligi hiyo ilianza tarehe 20 octoba 2014 na kushirikisha jumla ya timu 125 katika ngazi ya Kata, Tarafa na hatimaye Wilaya ikiwa na lengo la kuibua vipaji, kuboresha uhusiano na kujenga umoja, pamoja na kujenga afya na kwa wachezaji.
Timu nne za Cosmo ya Kiromba, Super Eagle ya mgao, Nanyamba kids ya Nanyamba na small boys ya Dihimba ndizo zilizofuzu kucheza hatua ya nusu fainali.

No comments: