Tuesday, November 4, 2014

UKWELI WAWEKWA WAZI JUU YA SAKATA LA MKE KUISHI NA WANAUME WAWILI ZAIDI YA MIAKA 8
Rogers na Juliana kwenye kikao cha usuluhishi


Hivi majuzi Mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Juliana Josia(22)alizua utata hivi karibuni baada ya kugunduliwa akiishi na wanaume wawili kwa muda wa miaka minane bila wanaume hao wawili  kujitambua.
Hayo yalibainika katika kituo cha Polisi cha Kati Jijini Mbeya baada ya Mwanamke huyo kudai kuporwa mtoto mgogoni jinsi ya kike mwenye umri wa miaka miwili eneo la Mwanjelwa Jijini Mbeya baada ya kutishiwa na Biton Bomani Mwashilindi mkazi wa Ilemi Jijini Mbeya.

Juliana alidai kuporwa mtoto na Biton Oktoba 27 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi alipokuwa akielekea soko la Sido kwenye shughuli zake za biashara na kutoa taarifa kituo cha Polisi Mwanjelwa na baadaye kituo kikuu kati na kufunguliwa jalada la wizi wa mtoto namba MB/RB/9384/2014 ambapo juhudi za kumtafuta zilifanikiwa baada ya taarifa kutolewa Kituo cha Radio cha Bomba FM Mbeya ndipo alipojisalimisha mwenyewe akiwa na mtoto Zalida Rogers(2).

Hata hivyo katika hali ya mshangao Biton alifika katika kituo cha Polisi Kati akiwa na Cheti cha kuzaliwa na kadi ya kliniki ambapo kinaonesha mtoto Zalida kuzaliwa kituo cha Afya Ruanda Mwanjelwa na kuonesha kuzaliwa 18/08/2012 wazazi wakiwa ni Juliana Josia na Biton Mwashilindi.

Biton alidai mbele ya Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi kuwa Juliana ni mpenzi wake kwa muda wa miaka nane na kwamba walikuwa wakikutana katika nyumba ya kulala wageni kila alipomhitaji na walikuwa wakipanga katika nyumba hiyo kwa siku saba kila wanapokutana hali ilyofanya watu wanaosikiliza tukio hilo kituo cha Polisi kushikwa na butwaa akiwemo mume halali Rogers Halinga na mke wa Biton ambaye alimtunza mtoto kwa siku nne.

Akijieleza kwa kujiamini Biton alidai kuwa hata mtaji wa biashara alimpatia yeye na hata wazazi wake Biton walioko Itaka Mbozi walimtambua mtoto Zalida na kwamba jina la mtoto alipewa na ndugu zake na hata aliowahi kuugua alikwenda Itaka Mbozi na kukaa kwa wazazi wa Biton kwa zaidi ya juma moja.

Kwa upande wa Rogers yeye alisema mtoto Zalida ni wa kwake na kwamba aliondoka kwao akiwana na ujauzito wa miezi mitano na kwamba yeye alijua kukorofishana kwao kulitokana na hali ya ujauzito na alikaa  kwamba mkewe Juliana alikaa kwao kwa miezi sita na alipojifungua alirejea kwake na aliohitaji kupata maendeleo ya mtoto mkewe alidai kuwa kadi ya kliniki imepotea.

Kikao hicho kilichokuwa na mvutano mkubwa kiliahirishwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya kwa kumshikilia Biton kwa kosa la kutorosha mtoto na kesi ya ugoni na kuwa atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika huku Rogers akikabidhiwa mkewe na mtoto kwa minajili ya kwenda kuyajenga huko nyumbani kwao Kijiji cha Ishungu Kata ya Ruiwa wilaya ya Mbarali.

Baba mzazi wa Rogers Mzee Jason Halinga alisema alishangazwa na kitendo kilichofanwya na mwanamke huyo ambapo alidai kuwa mwanae alioa kihalali na kufuata mila zote na kulipa mahari lakini alishangazwa na kitendo cha wazazi wa Juliana kushindwa kuonesha ushirikiano hali inayoashiria kujua kile kilichokuwa kinafanywa na mtoto wao.

Biton alifika kituo cha Polisi akiwa na mkewe wa ndoa ambapo naye hakufahamu kuwa mumewe anaishi na mke mwingine nje ya ndoa na kwamba mtoto Zalida alipoletwa kwake hakuambiwa chochote kile na kwamba ameishi kwenye mateso ya ndoa kwa muda wa miaka nane huku akifanyiwa vitendo vya kikatili na mumewe ikwa pamoja na kuambulia kipigo mara kwa mara.

Baadhi ya ndugu wa Rogers walioneshwa kukerwa na baadhi ya Askari wa ngazi  juu katika Dawati la Jinsia Kituoni hapo ambao walonesha kutojali suala hili huku wakitioa maneno ya kejeli hali inayotia dosari utendaji kazi wa Dawati hilo na kwamba lipo kibiashara zaidi na si  huduma kama ilivyo sera ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo hawakusita kuwapongeza Askari wa Kiume walionesha juhudi hata kufanikwa kupatikana kwa mtoto Zalida na Biton pamoja na rafiki yake.

Katika sakata hili kama si juhudi za Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ahmed Msangi kuingila kati basi mtoto Zalida asingeweza kupatikana kama baadhi ya watoto waliotoweka maeneo mbalimbali Mkoani Mbeya ambao hawajapatikana mpaka sasa ambapo wananchi wamelalamikia Kituo Kikuu cha Kati kwa kutochukua hatua za haraka za kukomesha vitendo vya ukatili wa Kijinsia na baadhi kuamua kumalizana wenyewe mitaani vikiwemo vitendo vya ubakaji ambavyo vimeshamiri mkoani Mbeya.

Sakata hilo limechukua sura mpya baada ya kikao cha ndugu wa mume halali Rogers Halinga kuketi Kijiji cha Ishungu Kata ya Ruiwa Mbarali Mkoani Mbeya na kumtaka Biton Mwashilindi kufanya mazungumzo nao kabla hawajafungua madai ya ugoni Mahakani na kudai fidia.

Kikao hicho kizito kilichofanyika nyumbani kwa Baba mzazi wa Rogers Halinga mzee Jason Halinga(95) Novemba mosi mwaka huu na kuhudhuriwa na ndugu lukuki na kumsikiza mke wa Rogers ili abaini ukweli juu ya mtoto aliyezua utata kuwa ni wa nani baina ya Rogers au Biton Mwashilindi.

Mwanamke huyo akijikanganya mara kadhaa katika kikao hicho akidai kuwa mtoto huyo ni wa Rogers kwa kuwa aliondoka baada ya kutokea mapishano na mumewe akiwa na ujauzito wa miezi minne ndipo alipoanza mahusiano ya kimapenzi na Biton hadi siku anajifungua mwaka 2012 akiwa mikononi mwa Biton ndipo alipoamua kumwandikisha mtoto katika kadi ya kliniki na cheti cha kuzaliwa jina la Biton.

Huku ndugu wakihamaki kutokana na kauli hiyo na kwamba yeye atamke wazi mtoto ni wa nani ndipo Juliana bila aibu kwa Baba Mkwe Mzee Jason Halinga alijibu kuwa mtoto ni wa Biton Mwashilindi,ambapo alimkabidhi mtoto huyo mwishoni mwa mwezi Octoba kwa hiari na wala hakuporwa kama alivyotoa taarifa Polisi.

Kauli hiyo ya Juliana ililazimu kikao kupiga simu kwa mzazi wa Juliana anayeishi Lwanjilo wilayani Chunya kujua mustakabali wa kauli ya mtoto wao kwani ilidaiwa kuwa Biton aliwahi kwenda huko kujitambulisha kuwa yeye anaishi na mtoto wao na kwamba Biton hakujua kuwa Juliana aliwahi kuolewa kwani alidai kuwa yeye ni mwanafunzi wa VETA Mbeya na asimwambie kuwa yeye ni mwanandoa.

Baba mzazi wa Juliana Hosea Mwalukasa alidai kuwa ni kweli Biton alifika kwake lakini hakumpokea kwa kuwa alidai kuwa Juliana ni mke halali wa Rogers Halinga hivyo kama amezaa na Juliana amefanya kosa na kwamba atatozwa ugoni kwani Juliana hakuwahi kupewa talaka na Halinga.

Kikao hicho baada ya mvutano wa muda mrefu kiliamua kuwa endapo Biton anadai kuwa mtoto aliyezaliwa na Juliana aliyefahamika kwa jina la Zalida Biton(2) ni mtoto wake basi alipe fidia ya kuzaa na mke wa mtu kiasi cha shilingi milioni kumi au alipe n'gombe saba ili aweze kumkomboa mtoto wake na kwamba Juliana bado ni mke halali wa Rogers.

Kwa upande wake Biton Mwashilindi alidai kuwa hayuko tayari kulipa pesa hizo na kwamba yeye alikabidhiwa mtoto kihalali na Jeshi la Polisi Ocktoba 31 mwaka huu kituo kikuu cha kati mbele ya maafisa wa Jeshi la Polisi na kwamba hana kesi ya kujibu na kwamba anasubiri tu mtoto afikishe umri wa miaka saba ndipo amchuke.

Katika suala hili baadhi ya wadau wamelalamikia Jeshi la Polisi kwa kuamua  masuala ya kisheria katika vituo vya Polisi badala ya mamlaka za kisheria zipo kama mahakama kuliko uamuzi uliotolewa na hali hii husababisha baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Wamedai kitendo cha kukabidhiwa mtoto Biton bila kuchukuliwa vipimo vya DNA bado hakujatutua mgogoro huu na kwamba bado suluhu katika ndoa hiyo hiyo itakuwa ni kitendawiri kisicho na majibu.

Na Mbeya yetu

No comments: