TUTAMNYIMA KURA BLATTER KATIKA UCHAGUZI WA FIFA
MWAKANI : UHOLANZI
CHAMA cha Soka cha Uholanzi-KNVB kimedai kutompigia
kura Sepp Blatter ambaye amethibitisha kugombea tena urais wa Shirikisho la
Soka Duniani-FIFA kwa kipindi cha tano. Rais wa KNVB Michael van Praag
aliwaambia waandishi wa habari kuhusu msimamo wao huo jana lakini akakiri kuwa
haoni kama kuna mtu anayeweza kumng’oa Blatter katika nafasi
hiyo. Uholanzi mara kadhaa wamekuwa wakimpinga Blatter mwenye umri wa
miaka 78 ambaye alichukua madaraka hayo kutoka kwa Joao Havelange mwaka
1998. Katika mkutano mkuu wa FIFA uliofanyika nchini Brazil kabla ya
kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia, KNVB ilimpasha Blatter kuwa anatakiwa
astaafu huku wakimtaka kuwajibika kutoka kashfa mbalimbali zilizolikumba
shirikisho hilo. Lakini Blatter anaonekana bado kutaka kuendelea kukomalia
nafasi hiyo kwa kipindi kingine kitakachomaliza mwaka 2019 akiwa na umri wa
zaidi ya miaka 83, baada ya rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA Michel
Platini kuweka wazi kuwa hatagombea kiti hicho. Praag amesema bahati mbaya
Platini amekataa kugombea kwani ndiye mtu pekee ambaye angeweza kusimama na
Blatter.
No comments:
Post a Comment