Friday, August 29, 2014

MCHUNGAJI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUISHI NA MKE WA MUUMINI WAKE 

Mchungaji Israel Mwakifuna

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, ambapo wananchi wengi wanaamini Mchungaji ni sehemu ya kukimbilia kueleza matatizo yao hususani migogoro ya kindoa, hali imekuwa tofauti jijini Mbeya.

Utata umeibuka baada ya Mchungaji, Israel Mwakifuna, wa Kanisa la Jeshi la Bwana(JB)lililopo Nzovwe jijini Mbeya amefikishwa katika Mahakama ya mwanzo ya Iyunga jijini Mbeya akituhumiwa  kuishi na mke wa mtu ambaye ni muumini wake.
Mchungaji huyo alifikishwa juzi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Iyunga, Nuru Lyimo akisaidiwa na Washauri wa mahakama Edson Mbeba na Rehema Haonga.
Kesi hiyo ya madai namba 51/2014 imepelekwa mahakamani hapo na  William Daimon Mwasubila(23)mkazi wa Nzovwe ambapo imedaiwa mahakamani Mchungaji kuishi na mke wake aitwaye Helena Mkea(21) kwa muda wa miezi minne sasa.
Mlalamikaji katika Kesi hiyo, Mwasubila aliiambia mahakama kuwa alikuwa akiishi na mkewe bila tatizo lakini matatizo yalianza pindi mkewe aliposhika ujauzito na kuamua kwenda kwa wakwe zake kwa matazamio baada ya mapishano yaliyodhaniwa kusababishwa na ujauzito hali ambayo alikubali.
Mwasubila alieendelea kuiambia mahakama kuwa mkewe alimuoa kihalali kupitia mshenga wake aliyefahamika kwa jina la Edward Mwangoje ambapo walifuata taratibu zote za mila kwa kulipa kiingilio cha mlangoni 50,000,kufungua 20,000,adhabu 50,000, kuku wawili, mashuka, mablanketi mawili na majembe mawili.
Alivitaja vitu vingine alivyolipia kama mahali kuwa ni mkaja wa mama 150,000 ambapo alilipa elfu hamsini,Mbuzi wawili jike na dume,n'gombe watatu dume ambao kila mmoja akiwa na thamani ya shilingi 300,000 na kupokelewa na wazazi kupitia kwa mshenga Octoba 20 mwaka 2013 eneo la Airport Jijini Mbeya.
Alisema mgogoro katika ndoa yao ulianza baada ya Mume kuzikuta SMS za mapenzi kwenye simu ya mkewe kwenda kwa mchungaji Mwakifuna ambapo alitoa taarifa kwa wazazi wapande zote mbili ambapo walijadili na kuondoa tofauti hizo na kuamua kuwasamehe.
Aliongeza kuwa  muda mfupi baada ya mazungumzo Mchungaji aliendelea kuwa na mahusiano ya kimapenzi na muumini wake hali iliyosababisha mke wa mchungaji Mwakifuna kuondoka kwa mumewe miezi minne iliyopita baada ya yeye(Mlalamikaji) kwenda kikazi Sumbawanga Mkoani Rukwa ambapo mkewe alihamia kwa Mchungaji wake na kuanza kuishi kama mke na mume.
Aliendelea kuiambia Mahakama kuwa Baada ya kutoka Sumabwanga  alipata taarifa kuwa mkewe anaishi na mchungaji ambapo aliamua kutoa taarifa Polisi kituo cha Nzovwe.
Alisema Jeshi la Polisi lilifika nyumbani kwa Mchungaji na Kumkuta  mkewe akiwa na mtoto wake wa kike mwenye umri wa wiki moja na nusu ndipo alipokamatwa  Agosti 25 na kufikishwa mahakamani Agosti 26, mwaka huu.
Baada ya kusikiliza shahidi mmoja wa upande wa mlalamikaji Hakimu Lyimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 3, mwaka huu mlalamikaji atakapoleta mashahidi wengine kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.
Mbeya yetu

No comments: