Thursday, July 31, 2014

AUAWA KWA KUCHOMWA VISU NA MCHUMBA WAKE

SIKU mbili kabla ya Sikukuu ya Eid el Fitr, binti aliyefahamika kwa jina la Salma Khamis (21) (pichani), amekumbwa na mauti kufuatia kuchomwa visu mwilini na mchumba wake aliyetajwa kwa jina la Omary Idd.
Tukio hilo lilitokea Julai 27, mwaka huu katika Kijiji cha Mnemela  wilayani Kibaha, Pwani kufuatia ugomvi wa mara kwa mara wa wawili hao unaosadikiwa ulitokana na wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mwanaume huyo alikuwa akimtuhumu Salma kwamba alikuwa na mwanaume mwingine mwenye gari, hivyo yeye akajiona hana chake ndiyo chanzo cha kuamua kumtoa uhai msichana huyo ambapo alimfuata kwa mama yake mkubwa alikokuwa na kumchoma visu mwilini hadi kufariki dunia.
Akisimulia tukio hilo la kusikitisha, baba mzazi wa marehemu Salma, Khamis Mbegu alisema kifo cha binti yake kimemuuma sana kwani ameuawa kinyama na siku alipopata taarifa hakuamini.
“Sikutegemea haya yaliyotokea, ni kweli walikuwa na ugomvi, wakaja kwangu kuwasuluhisha ndicho tulichokifanya, lakini  Salma alionesha msimamo wake wa kutokuendelea kuwa na Omary kwa sababu ya mateso na masimango aliyokuwa akimfanyia.
“Alishawahi kumpeleka porini na kutaka kumuua kama tu angesema hampendi, ikabidi aseme anampenda ili kuokoa uhai wake, hivyo alikuwa na shaka naye ndiyo maana hakutaka kuendelea na uchumba wao,” alisema baba huyo.
Aidha, ilielezwa kuwa mtuhumiwa ni mwenyeji wa Mkoa wa Singida, hivyo hata ndugu wa marehemu Salma hawajui anatoka kijiji gani wala kumtambua ndugu yake yeyote.
Kufuatia tukio hilo la mauaji, mtu mmoja anayedaiwa ni mshenga wa Omary, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa upelelezi zaidi.
Kamanda wa polisi wa mkoa huo, SACP  Ulrich Matei  alisema taarifa za kifo hicho amezipokea ambapo marehemu alichomwa visu sehemu mbalimbali za mwili na mtuhumiwa alikimbia lakini mshenga wake anashikiliwa kwa upepelezi zaidi kwa kuwa ndiye aliyekuwa ameongozana naye.
GPL

No comments: