Thursday, April 24, 2014

HUU NI UNYAMA, AFISA WA POLISI ADAIWA KUMUINGIZA CHUPA YA BIA SEHEMU ZA SIRI MKEWE MJAMZITO
MWANAMKE MMOJA mjamzito anauguza majeraha katika Hospitali ya Meru Level Five nchini Kenya baada ya kudaiwa mumewe aliingiza chupa kwenye sehemu zake za siri.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 31 alisemekana kupigwa na mumewe, ambaye anahudumu kama  Konstebo katika kambi ya polisi wa utawala ya Gatimbi, Kaunti ndogo ya Imenti.

Akieleza masaibu yake akiwa hospitalini, mama huyo  alisema mumewe aliyekuwa mlevi aliwasili nyumbani mwendo wa saa tisa alfajiri Jumamosi na kumwagiza avue nguo zote akiwa nje.

Alisema alitii maagizo hayo na polisi huyo akavaa sare yake ya kazi, akachukua chuma na risasi mbili kisha kumpiga na kusema kwa sauti kuwa ataua mtu siku hiyo.

 “Hapo ndipo alipochukua chupa ya pombe aliyokuwa amebeba na chuma, akaziingiza kwenye sehemu zangu za siri. Alinifunika mdomo ili nisipige kelele,” alieleza huku akidondokwa na machozi.

Alizimia kwa saa kadha ndani ya nyumba huku akivuja damu nyingi.

“Niliamka mwendo wa saa 11.30 na kumpata akiwa amelala kitandani, pengine alizidiwa na pombe nyingi aliyokunywa. Nilitambaa hadi makao makuu ya kambi ambapo maafisa wengine walinikimbiza hadi hospitalini,” alisema.

Baadaye alilazwa katika zahanati ya Gatimbi ingawa alihamishwa hadi hospitali ya Meru baadaye ili kupokea matibabu maalum.

Kulingana na Dkt Jamal Mohamed ambaye ni daktari katika hospitali hiyo, hayuko taabani kwa sasa ingawa bado anahitaji kutazamwa kwa makini.

 “Tunamtibu pia kutokana na matatizo ya kiakili aliyopata ingawa anaendelea vyema,” alisema.

Akithibitisha mkasa huo, Kamanda wa polisi wa utawala katika Kaunti ya Meru, Bw Njue Njagi, ambaye alimtembelea hospitalini alisema huenda wawili hao walikuwa na ugomvi wa kinyumbani kabla tukio hilo kutendeka.

Alisema mshukiwa huyo ambaye hakuwa amekamatwa wakati huo, atashtakiwa baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao.

Bw Njagi alisema afisa huyo ameagizwa kufika afisini na kuongeza kuwa agizo la kukamatwa kwake litatolewa ikibainika alikuwa na hatia.

“Hatujatambua kilichotokea kabla tukio hilo lakini uchunguzi unaendelea kulihusu. Atashtakiwa mahakamani ikiwa atapatikana na hatia,” alisema.

Mkuu huyo wa polisi aliomba maafisa wawe wakitafuta ushauri ili kuzuia matukio kama hayo kushuhudiwa.

Credit Swahili hub

No comments: