TAARIFA KUTOKA TFF LEO
WATANO WALALAMIKIWA KAMATI YA MAADILI
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati
ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili wa
waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi. Riziki Majala na Army
Sentimea ambao ni wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni
waamuzi wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha
taratibu.
Naye Sabri Mtulla analalamikiwa
na TFF kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa
hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi huku akijua
wazi kuwa jambo hilo si kweli.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko
hayo yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili kujiridhisha
kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo walalamikiwa watafika mbele ya
kamati hiyo.
TWIGA STARS, ZAMBIA KUCHEZA MACHI 2
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza
kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na
Zambia (Shepolopolo) itachezwa Machi 2 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam. Twiga Stars tayari imeingia kambini kujiandaa kwa
mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya
Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni
wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex. Shepolopolo iliibuka
na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka
huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka. Iwapo Twiga Stars itafanikiwa
kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe.
Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini. Wachezaji wa Twiga Stars
waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja,
Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya,
Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness
Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji,
Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.
STAND UNITED YAIKATIA RUFANI KANEMBWA JKT
Stand United ya Shinyanga imekata rufani Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) ikipinga Kanembwa JKT ya Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika
dirisha dogo kwenye mechi ya kiporo iliyozikutanisha timu hizo. Mechi hiyo
namba 22 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ilichezwa juzi (Februari 16 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na
ushindi wa bao 1-0. Katika rufani yake, Stand United inadai kwenye mechi
hiyo Kanembwa JKT ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika dirisha
kidogo kinyume na maelekezo kutoka TFF kwa timu hizo kuwa wachezaji
waliosajiliwa katika dirisha dogo hawawezi kucheza mechi hiyo. Wachezaji
wanaodaiwa kusajiliwa dirisha dogo na kucheza mechi hiyo ni Hamidu Juma,
Ibrahim Shaban Issa, Joseph Mlary, Lucas Charles Karanga, Raji Ismail,
Salvatory Kulia Raphael, Seif Ibrahim Zaid na Yonathan David Sabugowiga.
Dirisha dogo lilifunguliwa
Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani
yake inaombwa ipewe pointi tatu na mabao matatu kwa Kanembwa JKT kuchezesha
wachezaji wasiostahili. Awali mechi hiyo ilichezwa Novemba 2 mwaka jana
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, na kuvunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada
ya Kanembwa JKT kugomea pigo la penalti dhidi yao.
RAIS MALINZI AENDA KUJITAMBUSHA CAF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameondoka
leo (Februari 17 mwaka huu) kwenye Cairo, Misri kujitambulisha kwa uongozi wa
juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Akiwa Cairo, Rais
Malinzi ambaye alichaguliwa Oktoba 28 mwaka jana atakutana na Rais wa CAF, Issa
Hayatou pamoja na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Hicham El Amrani.
WATATU WAOMBEWA UHAMISHO WA KIMATAIFA
Wachezaji watatu wanaocheza mpira wa miguu nchini Tanzania wameombewa Hati ya
Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili wakacheze katika nchi za Thailand na
Ujerumani. Mchezaji Khamis Mroki Jamal aliyekuwa na timu ya Daraja la
Kwanza ya Polisi Dar es Salaam ameombewa ITC na Chama cha Mpira wa Miguu
Thailand (FAT) ili akajiunge na Kabinburi ya nchini humo. Said Ali Nassor
aliyekuwa akichezea FC Turkey ya Zanzibar na Samuel Chuonyo wameombewa na ITC
na Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DFB) kwa ajili ya kujiunga na klabu ya
VfB Eichstatt. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi
maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika ikiwemo ridhaa ya klabu zao
za hapa Tanzania itatoa ITC hizo.
No comments:
Post a Comment