Thursday, February 20, 2014

WANAWAKE WALIOBAKWA LIBYA KUFIDIWA
Waziri wa Sheria nchini Libya ,salaha al-Marghani,amesema kuwa Baraza la mawaziri limekubaliana kuwa Wanawake waliobakwa wakati wa maandamano na harakati za kuuangusha utawala wa aliyekuwa Rais wa taifa hilo Moammar Gaddafi mwaka 2011 watambuliwe kuwa waathirika wa vita.
Amesema makubaliano hayo yanayohitaji kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuwa Sheria yatamfanya mwanamke awe sawa na wale wapiganaji waasi waliojeruhiwa halikadhalika watalipwa fidia.
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu imekusanya ushahidi kuwa vikosi vya waliokuwa wakimuunga mkono Gaddafi walitekeleza vitendo vya ubakaji kama silaha.
Inaelezwa kuwa Wanawake wanaobakwa mara nyingi wamekuwa wakitengwa nchini Libya, hivyo haijafahamika wanawake wangapi watajitokeza.

WANAOVAA NUSU UCHI KWENDA JELA MIAKA 10 HUKO NCHINI UGANDA

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ametia saini sheria mpya inayotoa adhabu kali kwa watakaopatikana na hatia ya kutembea nusu uchi au kuhusika na vitendo vinavyohusisha picha zenye watu uchi.
Wanawake pia wamezuiwa kabisa kuvalia sketi fupi sana au ‘Mini Skirt’ kama zinavyojulikana au blausi ambazo zinaonyesha kifua chao hadharani na kusababisha hisia za kingono .
Sheria hiyo inasema kuwa nguo kama hizo zitakubalika tu ikiwa zinatumika
kwa ajili ya mafunzo au wakati wa michezo na hafla za kitamaduni.
Akihutubia waandishi wa habari, mjini Kampala, waziri wa maadili na utawala bora, Reverend Simon Lokodo alisema kuwa Rais Museveni alipitisha sheria hiyo tarehe 6 mwezi huu, miezi mwili bada ya bunge kuipitisha.
Kwa mujibu wa sheria hiyo kamati dhidi ya vitendo hivyo itabuniwa ili iweze kutekeleza sheria hiyo kwa kuhakikisha kuwa picha, au video zenye watu uchi zinanaswa na kuharibiwa. Kamati hiyo, itajumuisha watu kutoka katika sekta mbali mbali ikiwemo ya habari na utumbuizaji.
Sheria hiyo inasema kuwa mtu yeyote atakayepatikana akijihusisha na vitendo vya watu kuwa uchi, kuvalia nusu uchi , kuona sinema za watu wakiwa uchi au kuchapisha picha za watu walio uchi kwa lengo la kuleta hisia tofauti utachukuliwa hatua kali za kisheria.
Waziri alisema kuwa serikali haitaki watu kuvalia nguo zisizo na heshima na kuzua hisia zisizofaa miongoni mwa watu. Watakaopatikana wakivunja sheria na kuvalia visivyo watafungwa hadi miaka 10 na wale watakaopatikana na hatia ya kuhusisha watoto katika biashara ya ngono watafungwa hadi miaka 15.
BBC

No comments: