Friday, February 14, 2014

WAGANDA NA TANZANIA WATIA FORA KATIKA KUSHEREHEKEA VALENTINE UKILINGANISHA NA KENYA


ULIMWENGU mzima leo unaadhimisha Siku ya Wapendanao.

Utafiti uliofanywa Kenya, Uganda na Tanzania na kampuni ya Ipsos Synovate unaonyesha ni asilimia 65 pekee ya Wakenya waliohojiwa watakaosherehekea siku hii.

Hiyo ni kinyume na wenzao wa Tanzania (69) na Uganda (71).

Na hata kati ya hao watakaosherehekea, asilimia 23 wanasema hawatatumia zaidi ya Sh1,000.

Mkurugenzi Mkuu wa Ipsos Synovate, Bi Maggie Ireri, alisema hali hiyo inaibua maswali kuhusu kinachowasukuma Wakenya kutokuwa na hamu ya kusherehekea siku hii ya Velentino.

“Utafiti huu umeibua swali kubwa - je Waganda na Watanzania wana mahaba zaidi ya Wakenya? Ama ni gharama ya juu ya maisha inayoshuhudiwa Kenya ndiyo iliyoathiri jinsi watakavyotumia pesa katika siku hii?”

Kwa mfano asilimia 42 wanaotarajia zawadi za nguo ni kutoka Tazania. Uganda ni asilimia 36 na Kenya ni asilimia 31.

Kwa upande wa maua Waganda ni asilimia 37, Wakenya (36) na Watanzania (31).

Katika kusherehekea siku hii, Watanzania wana matumaini makubwa zaidi kwamba itakuwa iliyojaa mahaba kwa asilimia 72. Lakini Uganda na Kenya hawaamini hivyo. Kiwango cha wanaokubaliana na wenzao wa Tanzania ni asilimia 56 nchini Uganda na asilimia 52 pekee Kenya.

Hali hiyo pia inajitokeza miongoni mwa wale ambao hawana nia ya kusherehekea siku hii.

Utafiti huu unaonyesha kuwa watakaokosa kushehekea kwa sababu ya gharama ya maisha nchini Tanzania ni asilimia 58 wakifuatwa na Wakenya (asilimia 57) huku Waganda wakiwa asilimia 43.

Utafiti huu ulifanywa kati ya Februari 7 na 10 katika nchi za Kenya watu 1,050, Uganda (1,006) na Tanzania (528) mtawalia.

No comments: