Friday, February 14, 2014

HAPPY VALENTINE DAY
I LOVE YOU VALENTINE WANGU
Leo nimeona niongelee kidogo nini maana ya Valentine kwa asili yake kisha kila mtu kwa Imani yake na mapana yake akatambua kuwa anapokuwa sehemu ya Valentine Day anakuwa ana adhimisha nini maana wengi tunasheherekea Pasipo kujua asili yake.
Inaonekana maana halisi ya siku yenyewe inaharibiwa na watu wanaotumia fursa ya Valentine’s Day kufanikisha matakwa ya misukumo ya tamaa za miili yao.

Siku ya leo nchi zote za duniani hua zinaadhimisha siku hiyo ya wapendanao.

Ni wakati kama huu wa mwezi wa Februari ya kila mwaka ambapo maua husambazwa, wapenzi hupeana kadi za mapenzi, hutumiana sms za mahaba, kukiri makosa ya kimapenzi na kupeana miadi mipya ingawa haitekelezeki, yote hayo kwa lengo ni kuimalisha mapenzi baina ya wapendanao katika ‘Siku ya Wapendanao’ (Valentines’Day) Siku ya Februari 14.

Lakini , Jee tumeshawahi kujiuliza Valentine alikuwa nani na wapi utamaduni huo wa siku ya Valentine umetoka na nini malengo ya sikukuu hiyo?

HISTORIA YAKE FUPI

Historia yake imeanzia karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo padri Valentinus ambaye akaja kuheshimiwa kama mtakatifu hasa tarehe hiyo.

Inasemekana kwamba Kaisari wakati huo alikuwa Claudius II: yeye aliona kuwa askari mkakamavu na bora zaidi ni yule asiyeoa wala kuwa na familia (kapera). Hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari.

Valentinus alipinga jambo hili hivyo kuendelea kufungisha ndoa kwa siri. Mfalme Claudius alipopata habari hizi aliamuru Valentinus akamatwe na kuuawa.

Wakati  akiwa gerezani vijana wengi walikwenda kumtembelea, Valentinus aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu za kwanza za Valentine kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani; huyo binti inasemekana alikuwa ni wa askari jela na mara nyingi alikuwa anamtembelea kule gerezani.

Kabla anakwenda kunyongwa akaacha ujumbe wa barua ambao  mwisho wake alihitimisha kwa maneno haya: Kutoka kwa Valentinus wako. (From your valentine)

Toka hapo Valentine anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa kote duniani.

Aliyetangaza rasmi kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius.

Kwa hiyo kwa kifupi siku hiii inawahusu waliopo kwenye mapenzi hasa mwanamume na mwanamke.

Ingawa watu siku hizi wameichukulia kama ni kuonyesha upendo kwa  yeyote iwe baba, mama, kaka, mjomba si vibaya llakini hiyo siyo maana yake halisi.

Lakini pia baadhi ya watu wameibadilisha maana ya siku hii muhimu kwa wapendanao, na kuwa ni siku ya kufanya mambo yasiyofaa. Kwao, wapendanao ni ngono. Kuna ambao huanzisha uhusiano siku hiyo kwa lengo la kupata mtu wa kustarehe naye, hili ni kosa.

Kama mtazamo wako ni kutafuta mpenzi mpya na kwenda kustarehe naye utakuwa unakosea sana. Haina maana ya ngono wala anasa na kuharibu fedha kwenye ulevi. Yapo mengi ambayo unaweza kuyafanya kwa lengo la kuifanya siku yako kuwa nzuri.

Kama unafikiri unao upendo kwa watu basi bora hizo pesa ambazo ungezitumia kwa starehe basi nenda katoe msaada kwa wenye shida.
Katika jamii yetu kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wazee na wahitaji wengine. Tumia ulichojaliwa kushiriki nao utakuwa umeonesha namna unavyotambua umuhimu wa upendo.

Ifanye siku hiyo kuwa ya tofauti zaidi kwa kudumisha uhusiano wako na mpenzi wako na kuzungumzia changamoto mbalimbali za uhusiano wenu kuliko kuwaza starehe na anasa ambazo hupoteza fedha.

Ondoa fikra mbaya kichwani mwako rafiki, Waza kuhusu mema na kupendana kwa dhati, hapo utakuwa umekwenda sawa na maana ya sikukuu yenyewe.
Nawatakia velentine day njema kwa wale wanaojua maana.

No comments: