Tuesday, July 30, 2013

AFUNGWA MIAKA 14 JELA KWA KUZINI NA MBUZI
Picha kwa hisani ya Joachimjunior blog lakini haihusiani na tukio
MWANAMUME aliyepatikana na hatia ya kushiriki ngono na mbuzi amehukumiwa kifungo cha miaka 14 jela na mahakama Taita Taveta.
James Mbithe alishtakiwa kuwa mnamo Julai 9 katika kijiji cha Mgeno alifanya mapenzi na mbuzi anayemilikiwa na Bi Hannah Mambori.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Inspekta Peter Milimo ulisema mshukiwa alifumaniwa na mlalamishi aliyekuwa ameenda kuwaangalia mbuzi wake 12 waliokuwa machungani mita 300 kutoka nyumbani kwake.
Alimpata mshukiwa aliyemfahamu vyema akiwa amevua suruali ndefu yake huku mbuzi akitokwa na damu.
Baadaye aliripoti kisa hicho kwa mzee wa kijiji na baadaye kwa afisa wa matibabu ya mifugo ambaye alithibitisha kwamba mnyama huyo alikuwa amechafuliwa.
Mshtakiwa anadaiwa kumtendea mbuzi huyo kitendo hicho mchana kama adhabu baada ya kuingia shamba lake la mahindi na kuharibu mimea.
Mshtakiwa alikiri kosa hilo akisema hangeweza kukanusha kwa kuwa ulikuwa ndio ukweli.
Akijitetea, Mbithe, 59, aliomba ahurumiwe akisema ni mzee na kwamba alihadaiwa na shetani.
Akitoa hukumu, Kaimu Hakimu Mkuu Wundanyi Bi M. Chesang alisema kwa kuzingatia kujitetea kwa mshtakiwa, ripoti ya hali ya kiakili kutoka kwa Afisi ya Uchunguzi wa Hali za Kiakili, na sheria, mshtakiwa anafaa kutumikia kifungo cha miaka 14 jela.
Hukumu hiyo imetolewa chini ya wiki moja baada ya Idara ya Mahakama ndogo ya Taita kuzindua kampeni dhidi ya dhuluma za kimapenzi.
Hii ni baada ya polisi kusema asilimia 12 ya visa vya uhalifu vilivyoripotiwa kutoka eneo hilo kipindi cha miezi mitatu ni za dhuluma za kimapenzi.

No comments: