HALI YA MTWARA SASA YAANZA KUTENGEMAA TARATIBU BAADA YA JWTZ KUWASILI
KUANGALIA USALAMA, IDADI YA WALIOKUFA INAFIKIA 2
![]() |
Usalama wakiwa kazini Hospitali ya Ligula |
Hali ya usalama Manispaa ya Mtwara Mikindani inaanza kutulia baada ya kuwa tete juzi na jana kutokana na vurugu zilizokuwa zinaendelea mjini hapa.
Idadi ya waliokufa imeongezeka na kufikia wawili katika vurugu hizo ambapo jana mama mjamzito amekufa kwa kile kinachosemekana kupigwa risasi na polisi.
Habari zinadai kuwa mjamzito huyo ameuawa akiwa nyumbani kwake baada ya polisi kuvamia makazi yake.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi amethibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, zinazoaminika kuwa za risasi na hivyo kufanya idadi ya maiti zilizopokelewa hospitalini hapo kufikia mbili na majeruhi 18.
Mbali na hilo polisi pia wanadaiwa kuchoma moto nyumba tatu za wananchi katika mtaa wa Magomeni na vibanda vya maduka kadhaa na kupora vitu vilivyomo ndani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa amekanushwa tuhuma hizo za askari kuchoma nyumba moto na kupora mali, lakini ameahidi kufuatilia tuhuma hizo.
Hadi jana huduma za kijamii bado zilikuwa zimesimama, hakuna maduka yaliyokuwa wazi, hakukuwa na usafiri wa daladala wala pikipiki, mji ulikuwa kimya, sauti za milio ya mabomu na bunduki zilitawala, wanajeshi waliovalia sare waliuzingira mji wakiwa katika magari na pikipiki.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti wakazi hao wamelalamikia kitendo cha askali wa jeshi la polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga, na kuwapora mali zao .
Wakazi wa maeneo mbalimbali wamekimbia makazi yao hususani wanawake na watoto na kuhamia hospitali ya rufaa kwa kuhofia usalama wao huku wengi wao wakipotezana na ndugu zao.
Lakini mpaka leo asubuhi hali ipo shwari hakuna milio ya mabomu kama jana na watu wameanza kutembea maeneo mabalimbali ya mji huu kwa shughuli mbalimbali.
No comments:
Post a Comment