Wednesday, April 10, 2013

AFYA YAKO WIKI HII

KASI YA MAAMBUKIZI YA VVU MIKOA YA KUSINI YASHUKA



Mganga Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Dk Salum Rashid Kabuma, akitoa tathmini ya jinsi mkoa huo ulivyojipanga kukabiliana na Afya ya Uzazi wa mtoto, baba, na mama katika kukabiliana na maambukizi mapya ya VVU.

KIWANGO cha maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kimeshuka kwa kasi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kufuatia mwamko na ushirikiano wa dhati, kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa, katika kutekeleza sera ya afya ya uzazi.

Hadi kufikia sasa, takwimu zinaonesha kati ya watoto 100 wanaozaliwa na akinamama ambao tayari wamegundulika kuwa na maambukizi ya VVU ni watoto 2 huzaliwa na maambukizi, wakati wengine 98 huzaliwa wakiwa salama.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Dk Rashid Kabuma, aliyasema hayo ofisini kwake mkoani hapa, katika mazungumzo yake na maofisa watendaji kutoka Vodacom Foundation na Taasisi inayojishughulisha na Tafiti na Huduma za Afya ya Uzazi ya EGPAF.

Ujumbe huo ulikuwa katika ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo na ufanisi wa mashine 16 za kisasa zinazowezesha upatikanaji wa majibu ya vipimo vya VVU kwa watoto wachanga kwa haraka, zijulikanazo kama ‘sms printers’ kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, ambazo zimegharimu zaidi ya Dola za kimarekani elfu 23 zilizotolewa kama msaada na Vodacom Foundation, chini ya uratibu wa EGPAF.

Kabuma alibainisha kuwa siri ya mafanikio hayo ambayo yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa nchini kote, ni mwamko wa akinamama wajawazito katika kutambua mustakabali na thamani ya mtoto atakayezaliwa na namna bora ya kumuandalia mazingira salama kiafya.

“Kwakweli mwamko unaridhisha, na hata ukiangalia kiwango cha maambukizi ya VVU Mtwara ni asilimia 3.6 wakati akinamama wajawazito wenye maambukizi hayo ni asilimia 3.2 mwamko upo. Hivi sasa mama anapokuja kliniki anaongozana na baba na wote tunawapatia huduma na elimu stahiki juu ya Afya ya Uzazi,” alisema.

Hadi kufikia sasa mkoa wa Mtwara una idadi ya vituo 172 vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto ambapo kati ya hivyo vituo 85 sawa na asilimia 49 vinatoa huduma ya Afya ya uzazi. Na wazazi ambao wamepatiwa majibu ya vipimo kupitia sms printer wanafikia 107.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Dk Sonda Shaaban, alisema mkoa huo una idadi ya vituo 200 vinavyotoa huduma ya tiba na ushauri dhidi ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na takwimu zinaonesha wanawake waliopatiwa vipimo vya VVU ni 23924, na miongoni mwao 884 sawa na asilimia 3.7 waligundulika kuwa na maambukizi.

“Watoto wanaoendelea kufuatiliwa kwa ajili ya kupatiwa tiba endelevu mkoa wa Lindi ni 177 wakati wazazi ambao hadi sasa wamekwisha patiwa majibu ya vipimo vya vvu kupitia sms printer ni 71,” alisema Shaaban.

Naye Meneja wa Vodacom Foundation, Grace Lyon, alisema tangu Oktoba 2012 hadi sasa, Mfuko wa Kusaidia Jamii wa Kampuni yake umekwisha changia jumla ya sms Printers 43 katika mikoa kadhaa nchini, ikiwemo Shinyanga, Tabora, Arusha, Mtwara na Lindi.

“Tunatambua umuhimu wa huduma ya Afya ya Uzazi kwa mtanzania ndio sababu tumetoa msaada wa mashine hizi kuepusha usumbufu kwa wataalamu wa afya kusafiri umbali mrefu na kutumia muda mwingi kukusanya majibu ya VVU..hadi sasa tayari tumepeleka sms printers 9 Tabora, Shinyanga 5, Kilimanjaro 6, Arusha 6, Mtwara 8 na Lindi 8,” alisema Lyon.

No comments: