Wednesday, December 19, 2012

TFF YATHIBITISHA KUPOKEA BARUA KUTOKA ZFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limethibitisha kupokea barua ya Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ikieleza kuwafungia wachezaji kadhaa Wazanzibari wanaochezea klabu mbalimbali za timu za Tanzania Bara na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Suala hilo limepelekwa kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF kwa hatua zaidi, hivyo kwa sasa Shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo. Baadhi ya wachezaji hao ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Aggrey Morris, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis, Seif Abdallah na Selemani Kassim Selembe
Kamati ya Utendaji ya ZFA iliwafungia wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa kitendo chao cha kuamua kugawana zawadi ya Dola 10,000 walizopata baada ya kushinda nafasi ya tatu ya mashindano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) 2012 baada ya kuwafunga ndugu zao wa Tanzania Bara kwa penalti 6-5 mwezi uliopita nchini Uganda.

Licha ya ZFA kutangaza adhabu hiyo, wachezaji wote wameendelea kujifua katika klabu zao na hata timu ya taifa (Taifa Stars), jambo lililoonyesha kukichefua chama hicho cha soka cha Zanzibar, ambacho kimelalamikia kupuuzwa na TFF. 

Hata hivyo, maamuzi ya kuwafungia wachezaji hao kuchezea hadi klabu zao yamewashangaza wengi yakionekana kuwa ni ya jazba zaidi kwani chama cha soka hakiwezi kumzuia mchezaji kuitumikia klabu yake iliyomuajiri.  

No comments: