Tivo Vilanova
MADRID, Hispania KOCHA wa Barcelona, Tito Vilanova amerejewa na ugonjwa wa saratani katika vifuko vya kuhifadhia mate, gazeti la kila siku la Hispania la El Pais limeripoti leo likiegemea katika vyanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Vilanova (44), ambaye alifanyiwa upasuaji wa vifuko hivyo Novemba mwaka jana, alipanda ngazi kutoka katika nafasi yake ya ukocha msaidizi na kuchukua nafasi ya Pep Guardiola kama kocha mkuu msimu huu.
Vinara hao wa La Liga walitoa taarifa ya kufuta hafla yao ya Krismasi iliyopangwa kufanyika pamoja na vyombo vya habari na rais Sandro Rosell asubuhi ya leo, wakisema sababu zitatajwa baadaye. Vilanova alikuwa nje ya kazi yake kwa wiki tatu baada ya kufanyiwa upasuaji huo mwaka jana, lakini alirejea 'mzigoni' kumsaidia Guardiola katika miezi yake sita ya mwisho ya msimu wa 2011-12. Vilanova ameiwezesha timu yake kuongoza La Liga kwa kushinda mechi 15 kati ya 16, pointi tisa juu ya Atletico Madrid wanaoshika nafasi ya pili, na kutinga katika hatua ya 16-Bora ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kama vinara.
Barca imebakisha mechi moja, ugenini dhidi ya Valladolid katika La Liga Jumamosi, kabla ya mapumziko ya wiki mbili ya kupisha majira ya baridi
|
No comments:
Post a Comment