Wednesday, December 19, 2012

ZAMBIA WATUA DAR TAYARI KUIVAA TAIFA STARS JUMAMOSI

Nahodha Christopher Katongo ambaye juzi aliwashinda Didier Drogba wa Shanghai Shenhua na Yaya Toure wa Manchester City na kutwaa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika ni miongoni mwa nyota wa mabingwa wa Afrika, Zambia “Chipolopolo” waliotua jijini Dar es Salaam jioni hii kwa ajili ya kucheza mechi yao ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa “Taifa Stars” itakayipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Katongo na wenzake wametua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mishale ya saa 11:45, wakiwa pia na kocha  Mfaransa Herve Renard, ambaye ndiye aliyewasaidia kuishangaza dunia kwa kutwaa ubingwa wa Afrika 2012 katika fainali waliyoshinda kwa penati dhidi ya Ivory Coast nchini Gabon.
Mbali na Katongo, nyota wengine waliotua leo ni pamoja nyota wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rainford Kalaba na Given Singuluma ambaye ni  mfungaji bora wa fainali za kwanza za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).

Wengine ni Chintu Kampamba, Chisamba Lungu, Danny Munyau, Davy Kaumbwa, Derrick Mwansa, Evans Kangwa, Felix Katongo na Francis Kasonde, Hichani Himonde, Isaac Chansa, James Chamanga, Jimmy Chisenga, Jonas Sakuwaha, Joshua Titima, Kalililo Kakonje, Moses Phiri, Mukuka Mulenga, Rainford Kalaba, Roderick Kabwe na  Salulani Phiri.

Hata hivyo, beki Stopilla Sunzu wa klabu ya TP Mazembe ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mwaka 2012, si miongoni mwa wachezaji waliotua nchini jioni hii, leo Desemba 19, 2012 na haikuelezwa ni kwa sababu gani hayumo, tofauti na taarifa zilzotolewa awali.

KIINGILIO
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa kiingilio cha chini katika mechi hiyo ya Jumamosi itakayoanza saa 10:00 jioni kitakuwa Sh. 5,000 wakati cha juu kitakuwa Sh. 30,000

No comments: