DNA ZAONYESHA NUSU WA WATOTO NI WA KUSINGIZIWA
ASILIMIA 44 ya
wapenzi wanaokwenda Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupima vinasaba (DNA),
kwa ajili ya kujua uhalali wa watoto kwa baba, wamethibitishiwa kuwa watoto
hao si wa kwao.
Takwimu za mwaka
2012 kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, zimeainisha kuwa kati ya watu
90 waliokwenda kupima DNA, 40 ambao ni sawa na asilimia 44, wameonekana
kubambikiziwa watoto.
Takwimu hizo za
kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka huu, zilionyesha kuwa katika kesi 50 za
waliokwenda kupima, matokeo yalionyesha kuwa ni wazazi halisi wa watoto wao.
Hata hivyo, idadi
hiyo inayoonyesha kuwa kinababa siyo wazazi halisi wa watoto, imeshuka
ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2008/2009 ambazo zinaonyesha kuwa asilimia
60 ya watu waliochukua vipimo hivyo wamebainika kuwa si wazazi halisi wa
watoto hao.
Mkemia na Mtambuzi wa
Vinasaba vya Makosa ya Jinai, Gloria Machuve alisema jana kuwa ni vyema
ikitambulika kwamba takwimu hizo zinatokana na watu waliokwenda kupima baada
ya kutokea migogoro ya kimapenzi na siyo takwimu iliyochukuliwa kutoka kwa
Watanzania wote.
“Hatusemi kuwa
sasa wanaume wote Tanzania wanalea watoto ambao si wa kwao. Hizi ni
takwimu za waliokuja kupima; yaani wale wenye matatizo,” alisema.
Machuve alisema
katika maabara hiyo, kesi nyingi zinazoonyesha kuwa watoto hao si halali,
zimetokana na uhusiano wa ziada au usio rasmi baina ya wenza.
“Kwa mfano,
mwanamume ana mwanamke wa nje ya ndoa au mwenye uhusiano usio rasmi, halafu
mwanamke huyo anadai mtoto ni wa huyo mwanamume, mara nyingi matokeo
huwa si mazuri,” alisema Machuve.
Aidha, Machuve
alisema takwimu za kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 zinaonyesha kuwa tabia ya
upimaji imeongezeka miongoni mwa Watanzania.
Alisema mwaka
2005/2006, kesi za upimaji wa vinasaba zilikuwa 96 na mwaka 2008/2009 kesi
hizo zilikuwa 113 wakati mwaka 2009/2010, kesi za waliokwenda kupima
zilifikia 125.
Alisema watu wengi
wanaojitokeza kupima katika miaka ya karibuni wanataka kufahamu uhalali wa
watoto wao ili wawajibike kuwalea kihalali.
|
No comments:
Post a Comment