Tuesday, January 27, 2015

                 
KUNDI B la Mashindano ya Mataifa ya Afrika, AFCON 2015, limecheza Mechi zao za mwisho ambazo zote mbili ziliisha kwa Sare ambazo zimewanufaisha Tunisia na Congo DR kutinga Robo Fainali huku Cape Verde na Zambia wakitupwa nje.

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kusonga  hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja na Tunisia.
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesonga mbele baada ya kumaliza ikiwa ya pili kwenye kundi B nyuma ya Tunisia ambayo nayo pia imesonga mbele ikiwa ndio inayoongoza kundi hilo.
Pamoja na kwamba imemaliza ikiwa na pointi sawa na Cape Verde idadi kubwa ya magoli iliyofunga ndio iliyowavukisha.
Goli la pekee la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambalo ndilo lililowavukisha kusonga mbele lilifungwa na Jeremy Bokila. Na lile la Tunisia lilifungwa na Ahmed Akaichi.
Kwa upande mwingine timu nyingine kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na kati timu ya taifa ya Zambia Chipolopolo imefungasha virago kwenye mashindano hayo baada ya kumaliza ikiwa ya mwisho kwenye kundi hilo baada ya kutoka sare ya kutokufungana na Cape Verde.
Zambia ambaye ni Bingwa wa Kombe hilo mwaka 2012 na Cape Verde zote zimeyaaga mashindano hayo.
Zambia ilihitaji kushinda mechi hiyo japo kwa goli moja lakini bahati haikuwa yao kwani mwamwizi wa mpambano huo Néant Alioum alipopuliza kipenga cha mwisho matokeo yakabaki Zambia 0 Cape Verde 0.
Kwa matokeo hayo sasa Timu ya DRC itakutana na majirani zao  Congo Brazaville katika hatua ya robo fainali huku Tunisia wao wakikutana na wenyeji Equatorial Guinea
Wakati mashabiki wa huko Lusaka na maeneo mengine nchi Zambia wakiwa majozi kwa upande wao mashabiki wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao timu yao imesonga mbele wamekesha kwa furaha usiku kucha.

No comments: