KAMATI ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji imepitisha usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja
la Kwanza huku wenye kasoro ndogondogo klabu zao zikitakiwa kuziondoa ili
waweze kupatia leseni za kucheza ligi msimu huu wa 2014/2015. Kasoro hizo
ni kufikia makubaliano na klabu ambazo wachezaji husika wametoka, kuwafanyia
uhamisho (transfer) na kulipa ada za uhamisho. Kamati vilevile ilibaini
wachezaji wengi hawakufanyiwa uhamisho kama kanuni za ligi hizo
zinavyoelekeza. Hivyo, klabu ambazo hazitakuwa zimeondoa kasoro hizo kwa
wachezaji wao leseni zao zitazuiliwa mpaka watakapokuwa wamekamilisha kila
kitu. Ni wachezaji wenye leseni tu ndiyo watakaoruhusiwa kucheza mechi za
ligi.
Klabu za African Lyon, African
Sports, Ashanti United, Coastal Union, Kiluvya United, Majimaji, Mji Mkuu,
Polisi Dodoma, Polisi Morogoro, Red Coast na Stand United ziliwawekea pingamizi
wachezaji mbalimbali kwa kutofanyiwa uhamisho. Kuhusu Ike Bright Obina wa
Nigeria aliyewekewa pingamizi na African Lyon dhidi ya Coastal Union, Kamati
imezitaka klabu hizo kufikia makubaliano, na zikishindwa mchezaji huyo atabaki
African Lyon.
Kamati vilevile ilijadili
malalamiko ya Kocha wa zamani wa Simba, Zdravko Logarusic dhidi ya klabu hiyo,
na kuzipa pande hizo mbili siku 14 kufikia muafaka juu ya malalamiko hayo, na
zikishindwa ndipo zirejee tena mbele ya Kamati. Logarusic aliyewakilishwa
na mwanasheria wake Dickson Sanga anailalamikia klabu hiyo kwa kuvunja mkataba
kinyume cha taratibu, hivyo kutaka Simba imlipe dola 6,000 kwa kuvunja mkataba,
na pia kulipa dola 50,000 ikiwa ni fidia maalumu ya madhara yaliyotokana na
uvunjwaji huo.
No comments:
Post a Comment