Wednesday, July 16, 2014

TAARIFA KUTOKA TFF LEO


AFRIKA KUSINI YAWASILI KUIVAA SERENGETI BOYS
Afrika Kusini (Amajimbos) imewasili nchini kuikabili Tanzania (Serengeti Boys) katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 itakayochezwa keshokutwa (Julai 18 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo yenye msafara wa watu 37 ilitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana usiku (Julai 15 mwaka huu) na imefikia hoteli ya Sapphire. Amajimbos itafanya mazoezi leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Waamuzi watakaochezesha mechi hiyo kutoka Shelisheli wakiongozwa na Allister Barra tayari wamewasili nchini. Kamishna wa mechi hiyo ni Andriamiasasoa Doda Nirimboavonjy kutoka Madagascar.
Makocha wa timu za Seregenti Boys na Amajimbos pamoja na manahodha wao watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kiingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000. Tiketi zitauzwa uwanjani katika magari maalumu siku ya mechi.
SAMATA, ULIMWENGU WATUA, MWINYI KAZIMOTO KESHO
Washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wamewasili nchini leo asubuhi (Julai 16 mwaka huu) kutoka Tunisia kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji hao wamefikia hoteli ya Courtyard, Seaview Upanga na leo (Julai 16 mwaka huu) watafanya mazoezi kwa programu maalumu waliyopewa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij wakati wakiwasubiri wenzao.
Naye kiungo Mwinyi Kazimoto anayecheza mpira wa miguu katika klabu ya Almarhiya ya Qatar atawasili nchini kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 1.30 asubuhi kwa ndege ya Qatar Airways.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili Dar es Salaam kesho (Julai 17 mwaka huu) saa 3.20 asubuhi kwa ndege ya Fastjet kutoka Mbeya tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Msumbiji.
RAIS MALINZI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Ijumaa (Julai 18 mwaka huu).
Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) 

No comments: