Wednesday, June 11, 2014

WANANCHI NCHINI BRAZIL WASITISHA MAANDAMANO

Vuguvugu la watu wasio na makaazi nchini Brazil ambalo limekuwa likiunga mkono maandamano ya kupinga kombe la dunia sasa wametangaza kuwa wamesitisha maandamano hayo muda wote wa kombe la dunia .
Hii ni baada ya kufanikiwa kupata makubaliano na serikali, hata hivyo bado kuna wasiwasi kwa kuchipuza tena kwa mgomo wa wafanyakazi wa usafiri wa reli wa mjini uitwao 'Metro' ambao hawajapata uelewano na serikalii na wametishia kugoma tena kesho hadi pale madai yao ya nyongeza ya mshahara kwa 12% yatakapotekelezwa.
Kama kweli wakiendeleza vitisho hivyo basi itakuwa kasheshe kubwa mashabiki kusafiri hadi viwanjani kujionea mechi walizokuwa wakizisubiri kwa hamu kuu.
Mechi ya ufunguzi hapo kesho ni kati ya wenyeji Brazil dhidi ya Croatia.
Maandalizi ya kombe la dunia ya Brazil yamekumbwa na chelewachelewa na pia migomo ya makundi mbalimbali yanayotumia fursa hiyo ya kombe la dunia kudai nyongeza za mishahara na huduma bora za kijamii kutoka kwa serikali inayoshtumiwa kwa ufisadi na matumizi makubwa katika ujenzi wa viwanja na miundo mbinu kwa ajili tu ya kombe la dunia.

UCHAMBUZI MDOGO WA MICHUANO HIYO MWAKA HUU

Spain walichukuliwa kama moja ya Timu Bora Duniani Kihistoria baada kutwaa Mataji makubwa Matatu mfululizo lakini baada kipondo kikubwa huko Brazil Mwaka 2013 dhana hiyo ilififia.
Wakisifiwa na kutukuzwa kwa Staili yao ya ‘Tiki-Taka’ iliyowaletea Ubingwa EURO 2008, Kombe la Dunia 2010 na EURO 2012, ‘La Roja’ walibamizwa 3-0 kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara na ‘Wafalme wa Soka Duniani’ Brazil huko Maracana Stadium, Rio de Janeiro Mwaka 2013.
Kwenye Mechi hiyo, Kikosi cha Vicente Del Bosque kilicheza Staili yao ya kawaida ya ‘Tiki-Taka’ iliyojaa Pasi nyingi, fupi na za katikati ya Uwanja lakini Brazil, chini ya Luiz Felipe Scolari, ilicheza Staili ya moja kwa moja, kaunta-ataki za nguvu na haraka bila Pasi nyingi.
Akichambua kwenye Ripoti ya FIFA ya Kitaalam, Kocha wa zamani wa France, Gerard Houllier, ambae yupo Kamati ya Ufundi ya FIFA, ameeleza: “Tiki-taka imeleta matunda kwa Spain na Barcelona. Lakini kama huna Mshambuliaji ambae ni Sentafowadi wa kawaida na umechoka kwenye Hali ya Joto, mambo yatakuwa magumu kwako!”
Himaya ya Spain Duniani ilianza Mwaka 2008 huku Fernando Torres, akiwa kileleni mwa kipaji chake, akiongoza Mashambulizi yao.
Kuanzia 2010 zilianza kuonekana dalili kwa Timu pinzani za Spain kuweza kumudu Staili ya Spain kwa kujihami kwa kutumia Watu wengi nyuma lakini Spain, kwenye Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2010 huko Afrika Kusini, walifanikiwa kushinda Mechi 4 mfululizo kwa Bao 1-0 kila moja, ikiwemo Fainali, huku David Villa akifunga Mabao muhimu.
Hivi karibuni, Spain wamekuwa wakicheza bila kutumia Sentafowadi wa kawaida, Staili ya ‘Namba 9 wa Uongo’ [False 9], na Kiungo wao Cesc Fabregas akiwa ndie Mchezaji anaetumbukia mbele zaidi.
Huenda huko Brazil, kwenye Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka huu, Vicente Del Bosque asitumie Mfumo huo na badala yake kuwasimika Masentafowadi wa kawaida, Diego Costa au Fernando Torres au hata David Villa.
Vigogo wengine wa Soka Duniani, Germany, nao huenda wakatumia mfumo huo huo wa Spain wa kutokuwa na Sentafowadi wa kawaida kwani wanao Mastraika wawili tu huko Brazil, Miroslav Klose na Lukas Podolski.
Lakini Brazil, chini ya Big Phil, Luiz Felipe Scolari, wako tofauti kabisa.
Ikiwa watatumia Staili yao ya Kombe la Mabara, basi, bila shaka, Mashambulizi yao yatakuwa na Mtu 3 ya Fred, Hulk na Neymar, wakiongezewa nguvu na Mafulbeki wao wanaopanda juu, Marcelo na Dani Alves, kuleta Mashambulizi ya nguvu, kasi na kushtukiza.
Fowadi wa zamani wa Brazil, Zico, ameeleza: “Nategemea kuiona Brazil ikicheza staili ile ile ya Kombe la Mabara!”
Safari hii, Wachezesha Kamari wameipa Spain Nafasi ya 4 kutwaa Kombe la Dunia, nyuma ya Wenyeji Brazil, Argentina na Germany, hasa kwa vile Kikosi chao sasa ‘kimezeeka’ kikiwa na wastani wa Umri wa Miaka 29 na pia ‘kuzoeleka’ kwa ‘Tiki-Taka’ ambayo Beki wa zamani wa Manchester United na England Gary Neville ameiita: "Kumiliki bila Lengo".
Pengine, safari hii, lile Soka la Mpira wa ‘moja kwa moja’, Staili ya Timu kama England, inayotumia Chipukizi wenye mbio kama Viberenge, kina Daniel Sturridge na Raheem Sterling, huenda ikazaa matunda lakini swali kubwa ni, Je Hali ya Joto ya Brazil haitawaathiri?
Joto la Juu, na hasa unyevunyevu Hewani huwa Juu, kutazitesa sana Timu nyingi na hasa za Ulaya zilizozoea Baridi.
Miji ya Kusini huko Brazil, Rio, Sao Paulo na Curitiba, wastani wa Joto ni Nyuzijoto 20-25C lakini Kaskazini, kule Fortaleza, Salvador na Manaus, hugonga 25-30C, lakini kote unyevunyevu Hewani huwa Juu na hilo ndio tatizo kubwa.

No comments: