Monday, April 14, 2014

VODACOM WAIPONGEZA AZAM FC KWA UBINGWA BARA
Meneja Uhusiano wa Nje wa Kampumi ya Vodacom, Salum Mwalim

WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Bara, Vodacom imeipongeza timu ya Azam FC kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa 2013/2014.

Aidha, Vodacom imeipongeza Yanga kwa kushika nafasi ya pili pamoja na kuonyesha upinzani mkali kwa Azam katika mbio za kuusaka ubingwa ambao walikuwa akiutetea.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, mara baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Mbeya City na Azam FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Meneja Uhusiano wa Nje wa Kampumi ya Vodacom, Salum Mwalim amesema kwamba wakiwa wadhamini wameridhishwa na kiwango cha Azam FC na hivyo wanawapongeza kwa dhati.
Mwalim amesema Azam inabeba kwa mara ya kwanza ubingwa wa ligi tangu timu hiyo ilipoanza kushiriki Ligi Kuu mwaka 2008 na kwamba ushindi huo bila shaka utaongeza ushindani msimu ujao.
“Ubingwa wao huenda ukaifanya ligi ya mwakani kuwa ngumu zaidi, kwani timu za Yanga na Simba ambazo zimekuwa zikipokezana ubingwa kwa takribani miaka 20 zitataka kurudisha heshima yao na nyengine zikipata nguvu kuwa yeyote anaweza kuwa bingwa, iwapo atajipanga vyema kumudu ushindani, hilo likitokea ubora wa ligi utazidi kupaa.”
Amesema Azam watakabidhiwa Kombe lao la ubingwa April 19 kwenye Uwanja wa nyumbani kwao, Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam wakati wa mechi yao ya mwisho dhidi ya JKT Ruvu.
Akiizungumzia ligi, Mwalim amesema ilikuwa ya ushindani mkubwa na takribani kila mechi ilikuwa ngumu kwa kila timu, hali iliyolazimisha hata bingwa kujulikana kwenye mechi za mwishoni.

Aidha Mwalim amezipongeza timu zote 14 zilizoshiriki ligi hiyo kwa kujituma na kutoa changamoto katika kila mechi, jambo lililofanya bingwa kutopatikana kwa urahisi na mapema.
Pia amezipongeza Mbeya City kuwa ni timu iliyoleta changamoto mpya kwenye ligi hiyona kuipa afya zaidi na anaamini itakuwa mfano tosha kwa timu nyingine msimu ujao.

Amesema awali Mbeya City ilionekana kama imeingia na nguvu ya soda, lakini kadiri ligi ilivyokuwa ikosonga mbele, ilionyesha kuwa imedhamiria kufanya vyema huku ikihimili mikikimiki yote ya ligi na hivyo kuifanya kuwa timu inayohitaji kupewa sifa za kipekee kwa msimu huu.
Vodacom imewapongeza pia wakazi na wenyeji wa mkoa wa Mbeya kwa kuiunga mkono timu yao kwa hali na mali na hivyo kuipatia mafanikio huku hatua yao hiyo ikinogesha pia joto la ligi ndani na nje ya mkoa wa Mbeya.
Kwa kutwaa Ubingwa huku wakiwa na Mechi 1 mkononi, Azam FC imefuta kuhodhi kwa Ubingwa kwa Vigogo Yanga na Simba tangu Mwaka 2001 ambapo, baada ya Mtibwa kuutwaa Mwaka 2000 na kuutetea Mwaka 2001, Yanga na Simba zimekuwa zikipishana kwa kuubeba.
VPL itakamilika Wikiendi ijayo Aprili 19 kwa Timu zote 14 kuwa Dimbani.
MSIMAMO-Timu za Juu:
NA
TIMU
P
W
D
L
GD
GF
PTS
1
Azam FC
25
17
8
0
35
50
59
2
Yanga SC
25
16
7
2
42
60
55
3
Mbeya City
25
12
10
3
12
31
46
4
Simba SC
25
9
10
6
14
40
37

No comments: