ALAZIMIKA KUTEMBELEA
MKEWE MOCHARI KILA WIKI ILI
KUEPUKA KUSUMBULIWA USIKU AKILALA
![]() |
Bw Erick Guni Mwatela |
MWANAMUME
kutoka Kinango, Kwale nchini Kenya ambaye amekatazwa na wakwe zake kumzika mkewe aliyefariki
zaidi ya miaka miwili iliyopita sasa anasema amelazimika kumtembelea mochari
kila wiki ili kuepuka kusumbuliwa usiku akilala.
Bw
Erick Guni Mwatela, mwenye umri wa miaka 28, ana kibarua cha kuzuru chumba cha
kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya Pwani, Mombasa ili kuona mwili wa mkewe
ambaye anasema si mwili tena kutokana na muda mrefu ambao umekuwa hapo.
Ninalazimika
kwenda katika chumba hicho kwa sababu nikikosa mke wangu marehemu Francisca
Wawuda hunifuata nikilala na kutaka kujua ni kwa nini nimemuacha,”
Bi
Wawuda alifariki mnamo Februari 2012 akijifungua na sasa Bw Mwatela amebaki na
mwanawe wa kike aliyezaliwa siku ya kifo hicho.
Alisema
alikutana na mkewe akifanya kazi katika kiwanda cha EPZ eneo la Mazeras,
wakachumbiana kisha wakaoana.
“Mke
wangu aliniambia yeye ni yatima. Nyanya yake pia alisisitiza hilo na dada yake
mkubwa pia akasema wao yatima. Lakini niligundua ana baba nilipoenda mochari
kuchukua mwili wake ili kuuzika. Watu ambao sikuwajua walijitokeza na kusema
sisi ni wezi wa maiti,” akasema.
Akaongeza:
“Kulizuka kizaazaa kikubwa na hata tukaenda kortini. Kinachosikitisha ni kwamba
tunapozozana, mwili wa mke wangu unaendelea kuoza na gaharama ya mochari
inapanda kila siku.”
Gharama
ya kuhifadhi maiti hiyo sasa imefika Sh350,000.
Jadis
Munga ambaye ndiye baba ya marehemu Wawuda, anasisitiza ndiye anayestahili
kumzika bintiye akisema Mwatela hakulipa mahari mkewe alipokuwa hai.
Alishinda
kesi kortini lakini alipoenda kuchukua mwili kuuzika akapata barua ya kumzuia
kuuchukua.
“Nakumbuka
nyanya ya marehemu akimuuliza baba yake sababu yake kuninyima mwili ilhali yeye
pia hakulipa mahari. Sijui ni kwa nini anafanya hivyo. Naomba kusaidiwa,”
akasema Mwateka na kuongeza kwamba alilazimika kuziba kaburi alilokuwa
amechimba kumzika mkewe.
Alisema
alilipa Sh5,000 za 'kifungua mlango’ kwa nyanya ya marehemu ndipo akawapa
idhini ya kuishi kama mume na mke.
Mnamo
2011, mkewe alipata mimba lakini akapata matatizo wakati wa kujifungua.
Alilazwa katika hospitali ya wilaya ya Port Reitz mjini Mombasa na baadaye
akahamishwa hadi hospitali kuu ya Pwani ambako alifariki Februari 27, 2012.
Bw
Mwatela anaomba serikali imsaidie kulipa deni la mochari na kuingilia kati
suala hilo ili mkewe azikwe.
Anasema
Kenya inafaa kuwa na korti maalumu ya kushughulikia kesi za kimila, ada na
desturi za jamii za humu nchini.
“Kuna
kitu ambacho kinafichwa. Ni kwa nini baba mkwe anasisitiza anataka mwili wa mke
wangu ilhali aliwatoroka? Ama ni mwanachama wa chama kimoja cha jamiiya
Wachonyi chenye desturi mbaya inayoitwa wala watu?” akauliza.
Bw
Munga anasema kulingana na mila ya jamii ya Wachonyi, mwanamke ambaye
hajajulisha wazazi wake kwa mchumba ama mume wake huwa hajaolewa. Kwa hivyo
mume hana idhini ya kumzika hadi pale atakapotimiza mila hiyo.
Hata
hivyo anasisitiza kuwa hataki hata ndururu ya Bw Mwatela kwa kuwa kimila
bintiye hakuwa ameolewa.
Taifa leo
Taifa leo
No comments:
Post a Comment