Friday, January 31, 2014

SANTANDER WAGOMEA MECHI BAADA SEKUNDE 40 COPA del REY


WACHEZAJI wa Racing Santander Usiku wa kuamkia leo wamegomea Mechi ya Marudiano ya Robo Fainali ya Copa del Rey dhidi ya Real Sociedad Sekunde 40 tu tangu Mechi hiyo ianze.
Kabla ya Mechi, Wachezaji hao walitoa onyo kuwa watagomea Mechi hiyo ama Rais wa Klabu hiyo, Angel Lavin, na Bodi yake ijiuzulu kwa sababu ya kutolipwa Mishahara yao.
Hata hivyo, Wachezaji hao waliingia Uwanjani na kupasha moto kabla Mechi kuanza na baadae Refa Jesus Gil akaamuru Mechi ianze na Real Sociedad walianza kucheza Mpira lakini Wachezaji wa Racing Santander walisimama kwenye Duara la Kati huku wakikumbatiana kitendo kilichowafanya Sociedad wapasiane Mpira kwa Dakika mbili upande wao wa Uwanja na kisha kuutoa nje uwe Mpira wa Kurusha.
Wachezaji wa Sociedad walikataa kurusha Mpira huo na Refa Jesus Gil akavunja Mechi hiyo.
Wachezaji hao wa Racing Santander, ambayo iko Daraja la chini huko Spain, wanadai hawajalipwa Mishahara kwa Miezi kadhaa sasa.
Mara baada ya Mechi kuvunjwa Wachezaji wa Sociedad waliwakumbatia wenzao huku Mashabiki wa Santander, ambao walikuwa Uwanja wa Nyumbani, wakishangilia.
Katika Mechi ya Kwanza ya Robo Fainali, Real Sociedad iliichapa Racing Santander Bao 3-1 na ni wazi watapewa ushindi kwenda Nusu Fainali kucheza na Barcelona.

No comments: