Monday, January 13, 2014

MAPINDUZI CUP LAENDA UGANDA, SIMBA YALALA 1-0 
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein akikabidhi Kombe la ubingwa kwa KCC
Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar

BAO pekee la Herman Wasswa, limeipa KCC ya Uganda ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2014, baada ya kuilaza Simba SC 1-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni hii. 
Waswa alifunga bao hilo dakika ya 20 baada ya kumhadaa beki wa kushoto wa Simba SC, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na kufumua shuti lililompita kipa Ivo Mapunda aliyekuwa amezubaa.
Pamoja na kurejea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa nyuma kwa bao 1-0, lakini Simba SC walicheza vizuri isipokuwa bahati haikuwa yao.
Safu ya ulinzi ya KCC ilikuwa imara mno leo kuwadhibiti washambuliaji wote wa Simba SC hadi mwisho wa mchezo. 
Kipindi cha pili, Simba SC ingeweza kufungwa bao la pili kutokana na wachezaji wake wote kwenda kushambulia na KCC wakawa wanatumia nafasi hizo kufanya mashambulizi ya kushitukiza yaliyokuwa hatari.
Lakini nao Simba SC katika kushambulia kwao walikosa mabao ya wazi kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini katika kumalizia nafasi nzuri walizotengeneza.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein alimkabidhi Kombe la ubingwa wa Mapinduzi na fedha taslimu, Sh. Milioni 10, Nahodha wa KCC, Fahad Kawooya.
Simba SC walipewa Sh, Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili, wakati mchezaji Tony Odur wa KCC alipewa king’amuzi cha Azam TV kwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.  
Mkurugenzi wa CXC Safaris & Tours ya Dar es Salaam, Charles Hamkah alikabidhi Sh. 300,000 kwa kila mmoja, mfungaji bora Owen Kasuule wa URA, mchezaji bora Mwinyi Mngwali wa Cloves Stars na kipa bora, Ivo Mapunda wa Simba SC. 
Kwa kutwaa ubingwa huo, KCC inakuwa timu ya kwanza kutoka nje ya Tanzania kubeba taji hilo na bingwa wa nane kihistoria wa Kombe la Mapinduzi. 
Sasa ni timu sita zimetwaa Kombe hilo tangu limeanzishwa mwaka 2007, Yanga SC ya Dar es Salaam ikikata utepe, ikifuatiwa na watani wao, Simba SC (2008), Miembeni ya hapa (2009), Mtibwa Sugar ya Morogoro (2010), Simba SC tena 2011 na Azam FC mara mbili mfululizo 2012 na 2013 na KCC mwaka huu.
Mabingwa watetezi, Azam safari hii wamekwamia kwenye Nusu Fainali baada ya kutolewa na KCC kwa kufungwa mabao 3-2, ikitoka nyuma kwa 2-0. 

No comments: