Wednesday, December 4, 2013

MAAJABU YA ULIMWENGU, MBWA AZAA  SUNGURA NA KUMNYONYESHA HUKO KENYA
Mbwa akiwa na mwanasungura
WENYEJI wa kijiji cha Kithenge kutoka wilaya ya Igembe kusini nchini Kenya wamebaki vinywa wazi kufuatia tukio la kustaajabisha ambapo mbwa amejifungua sungura badala ya mbwa wa kawaida.

Kulingana na  mwenye mbwa huyo Bw Josphat Kairithia, kitendo hiki kilitokea Jumanne wiki iliyopita ambapo alimkuta mbwa huyo akimyonyesha na akadhania ni mbwa wa kawaida.
Baada ya kuchunguza zaidi, aligundua kuwa hakuwa mbwa wa kawaida bali sungura na hapo ndipo alianza kuwaita majirani waje kushuhudia tukio hilo.
Hata hivyo, waliokuja walishtuka zaidi na wengine wakitoroka wakidhania kuwa hayo yalikuwa mazingaombwe.
Kairithia aliongeza kuwa mbwa huyu aliendelea kumnyonyesha sungura huyo kama kawaida na kumpa ulinzi wa mwana.
“Tukio hili limenishangaza sana na siwezi nikaeleza kilichotendeka. Anamnyonyesha sungura huyu kama kawaida na hataki kumuona mtu akimkaribia. wanaokuja kumwona lazima wapitie kwangu ili niweze kumtuliza mbwa huyo la sivyo wakiona  cha mtema kuni,” akasema.
Kairithia alitupilia mbali uwezekano kuwa hayo yangekuwa mazingaombwe huku akielezea kuwa  huenda ikawa ni ujumbe kutoka kwa mungu kuwaambia watu wapende maadui wao.
“Siwezi nikasema kuwa haya ni mazingaombwe kwani najua ya kwamba mungu ana njia nyingi za kuongea na watu wake. Labda anataka kutuelezea jinsi ambavyo tunapaswa kuwapenda hata wale ambao tunafikiri ni maadui wetu,” akasema.
Ametupilia mbali fununu za watu ambao wanadai kuwa huenda alimwekea mbwa huyo sungura huyo akisema kuwa hakuwa karibu mambo hayo yakitendeka.
Ili kutoa thibitisho kwa watu, Kairithia alimwekea sungura mwingine karibu na mbwa huyo na kilichowashangaza wengi ni kuwa hakupoteza muda kumla.
Mamia ya watu wanazidi kutembelea familia hiyo kwa nia ya kuyaona maajabu hayo ya ulimwengu.

 

No comments: