BAADA YA USHINDI WA 2-1, MOURINHO AMLAUMU
SUAREZ KWA KUJIRUSHA KAMA YUPO BWAWA LA KUOGELEA, BRENDAN RODGERS ATETEA.
![]() |
Brendan Rodgers kushoto na Jose Mourinho kulia |
MENEJA wa
Chelsea Jose Mourinho amesema Straika wa Liverpool Luis Suarez alipaswa kupewa
Kadi za Njano kwa kujiangusha kwenye Mechi ya Jana Usiku Uwanjani Stamford
Bridge ambayo Chelsea iliitwanga Liverpool Bao 2-1.
Katika moja ya matukio ya Suarez ni pale alipokuwa akimfukuza Cesar Azpilicueta ndani ya Boksi na kugongana na Samuel Eto'o na hilo limemkera Jose Mourinho aliesema: “Hakuzongwa. Suarez alizidiwa maarifa na Azpilicueta ambae alikuwa na Mpira huku akitoka nje ya Boksi. Suarez akaamua kujirusha kama vile anadaivu kwenye Bwawa la Kuogelea!”
Mourinho aliongeza: “Ni mjanja kwani anajua yuko kwenye Boksi na nyuma ya Goli wapo Mashabiki wa Liverpool! Lakini Refa Howard Webb alikuwa Mita 10 tu na nadhani kosa pekee alilofanya ni kutompa Kadi ya Njano Suarez!”
Tukio hilo lilitokea katika Dakika za mwisho za Mechi ambayo Liverpool walitangulia kufunga kwa Bao la Martin Skrtel na Chelsea kujibu kwa Bao za Eden Hazard na Samuel Eto'o.
Pia Mourinho alieleza: “Siku zote nafurahi kumuona Suarez kwani ana Kipaji, anajituma na ana ari ya ushindi. Ni Mchezaji Bora. Lakini Nchi hii ni spesho. Mimi si Muingereza lakini nina wajibu kutetea thamani ya Soka hapa. Kitu kimoja bora tunacho hapa ni kuwa Watu hawapendi kuhadaa. Ile hali iliyokuwepo kati ya yeye na Azpilicueta na Eto'o ni lazima ikome au apewe Kadi za Njano kwani si kitu chema kwa Soka letu.”
Suarez, ambae ni Raia wa Uruguay, Msimu huu amefunga Bao 19 katika Mechi 14 tangu arejee Kiwanjani akitokea kwenye Kifungo cha Mechi 10 kwa kumuuma Meno Beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic, Mwezi Aprili kwenye Mechi kati ya Liverpool na Chelsea.
Hata hivyo, Meneja wa Liverpool, Brendan Rodgers, ambae alikuwa Msaidizi wa Jose Mourinho kati ya Miaka 2004 na 2007 wakati wa himaya ya kwanza ya Mourinho huko Chelsea kwa mara ya kwanza, alikuwa na mtazamo tofauti na hasa tukio la Eto’o kumchezea faulo Jordan Henderson iliyoleta Frikiki iliyozaa Bao la Skrtel.
Rodgers amedai: “Ilipaswa Eto'o apewe Kadi Nyekundu! Najua tumefunga kwa faulo yake lakini ile ni rafu mbaya na hakupata hata Kadi ya Njano!”
Kuhusu Suarez, Brendan Rodgers ameeleza: “Luis Siku zote atasababisha Mabeki wamvae, ndio maana yuko kiwango cha juu Duniani. Kitu ambacho hakutegemea ni kugongwa na Mtu ambae hana Mpira. Pale alikuwa akikimbia kumkabili Azpilicueta na Eto'o ana ujanja wa Mtaani, alifanya safi, alimziba Suarez. Siku nyingine unaweza kutoa ile iwe Penati kwa sababu amemzuia!”
Brendan Rodgers alimalizia: “Ni dhahiri, Mourinho atamtetea Mchezaji wake na mimi nitamtetea wangu!”
No comments:
Post a Comment