YALIYOJIRI KUELEKEA KOMBE LA DUNIA 2014 NCHINI BRAZIL
MACHO na masikio ya mashabiki
wa soka barani Afrika yatakuwa yakitizama mechi tano muhimu zitakazochezwa
Jumamosi, Jumapili na Jumanne ambazo ndio zitakazotoa wawakilishi watano
watakaoliwakilisha bara hili katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini
Brazil. Jumamosi tutashuhudia Ethiopia ikisafiri kuifuata Nigeria ili
kujaribu kurekebisha makosa ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza wakati
huko jijini Casablanca, Morocco, Senegal itaikaribisha Ivory Coast ambao
walishinda mechi ya kwanza iliyofanyika jijini Abidjan kwa mabao
3-1. Jumapili kutakuwa na mtanange mwingine wa kukata na shoka ambapo
Tunisia wataifuata Cameroon jijini Younde baada ya kwenda sare ya bila ya
kufungana katika mchezo wa kwanza uliofanyika Octoba. Ratiba hiyo
itakamilika Jumanne ambapo Misri itakuwa na kibarua kigumu jijini Cairo cha
kugeuza matokeo ya bao 6-1 walizochapwa na Ghana katika mchezo wa kwanza
uliofanyika jijini Kumasi wakati Burkina Faso nao wakijaribu bahati yao mbele
ya Algeria baada ya kuwafunga mabao 3-2 katika mechi ya kwanza.
GHANA WAOMBA KUONGEZEWA ULINZI ZAIDI.
MAAFISA wa Shirikisho
la Soka la Ghana-GFA limewaomba wenyeji wao Misri ulinzi zaidi kama tahadhari
wakati timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Black Stars itakapowasili jijini
Cairo wiki ijayo. Maofisa wanne kutoka GFA waliwasili jana Misri kwa ajili
ya kufanya mazungumzo na viongozi wan chi hiyo pamoja na kupata taarifa ya
usalama pamoja na wawakilishi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Mjumbe
wa bodi wa Shirikisho la Soka la Misri, Ehab Laheita ambaye alihudhuria mkutano
huo amesema maofisa hao wa Ghana waliomba ulinzi zaidi wakati timu yao
itakapowasili jijini Cairo na muwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Ndani
aliwahakikishia hilo. Laheita aliendelea kudai kuwa viongozi hao walikagua
Uwanja wa Air Defense utakaotumika kwa ajili ya mchezo huo na kuridhishwa nao
na kuomba nafasi zaidi kwa ajili ya mashabiki wao. Maofisa hao waliongozwa
na rais wa GFA Kwesi Nyantakyi, Abeid Ayew Pele, Alhaji Saeed Lartey na Ibrahim
Sannie.
ETO'O ALALAMIKIA WACHEZAJI WENZAKE CAMEROON KUMBANIA.
MSHAMBULIAJI nyota wa
klabu ya Chelsea, Samuel Eto’o anaamini kuwa baadhi ya wachezaji wenzake wa
Cameroon wanajaribu kutomsaidia asishinde katika mechi yao ya mtoano ya Kombe
la Dunia dhidi ya Tunisia. Kauli hiyo ya Eto,o imekuja wakati wakielekea
katika mechi ya mkondo wa pili itakayofanyika jijini Younde baada ya ile ya
kwanza iliyofanyika jijini Tunis Octoba timu hizo kwenda sare ya bila ya
kufungana. Eto’o mwenye umri wa miaka 32 amedai kuwa wachezaji wenzake
wamekuwa hawapeleki mipira ipasavyo anapokuwa mbele hivyo inampasa kurudi nyuma
zaidi ili kwenda kutafuta mipira mwenyewe. Nyota huyo aliendelea kudai
kuwa soka ni mchezo wa ushirikiano na mchezaji ana jukumu la kutoa pasi hata
kama unayempa mpira huo ni adui yako hususani unapokuwa katika nafasi
nzuri. Hata hivyo, kocha wa Cameroon Volker Finke amepinga vikali madai
hayo ya Eto’o na kusisitiza hakuona tatizo kama hilo wakati wa mchezo wao
uliopita waliotoka sare.
WACHEZAJI CROATIA KUMWAGIWA FEDHA KAMA WAKIFUZU KOMBE LA DUNIA.
SHIRIKISHO la Soka
nchini Croatia limetoa kitita cha euro 500,000 kama motisha kwa wachezaji wa
timu ya taifa ya nchi hiyo kama wakifanikiwa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia
itakayofanyika mwakani nchini Brazil. Croatia inakabiliwa na mechi mbili
za mtoano dhidi ya Iceland ili kukata tiketi kwa ajili ya michuano
hiyo. Mechi ya mkondo wa kwanza kati ya timu hizo inatarajiwa kuchezwa
jijini Reykjavik baadae leo huku mechi ya mkondo wa pili ikitarajiwa kuchezwa
jijini Zagreb Jumanne ijayo. Croatia ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya
tatu kwenye michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1998 iliyofanyika nchini Ufaransa
lakini walishindwa kufuzu michuano iliyopita ambayo ilifanyika nchini Afrika
Kusini.
No comments:
Post a Comment