Friday, November 15, 2013

ALIYEBAKA PUNDA AFUNGWA JELA MIAKA HUKO NCHINI KENYA
James Mwangi
MAHAKAMA ya Nyeri nchini Kenya jana imemhukumu mwanaume aliyepatikana na hatia ya kushiriki kitendo cha ngono na punda miaka sita jela.
James Mwangi alipatikana na hatia ya kutenda kosa hilo Aprili 26 katika kijiji cha Ruring’u maeneo ya Nyeri na kulingana na Hakimu mkuu wa Nyeri Bi Wilbroda Juma, mashahidi walitoa ushahidi wa kutosha kudhihirisha kuwa Mwangi alishiriki kitendo hicho
Bi Juma alisema kuwa mwenye punda Bw Peter Mathenge, alikuwa mmoja wa mashahidi na alieleza mahakama hiyo kuwa alimwacha punda huyo na punda wengine wachanga malishoni lakini akafahamishwa baadaye na jirani kuwa Mwangi alipatikana akifanya kitendo hicho kwa punda huyo.
Bw Mathenge alisema kwamba alielekea katika eneo alimokuwa ameelekezwa na jirani yake na kupata mipira ya kondomu katika eneo ambalo punda wake alitendewa uovu huo. Hapo ndipo aliamua kuwafahamisha maafisa wa polisi.
Maafisa wa polisi pia walitoa ushahidi katika mahakama hiyo na kuelezea kuwa walimhoji mmoja wa walioshuhudia tukio hilo aliyejitambulisha kama Bw Ng’ang’a na akasema kwamba aliona punda huyo akiwa amefungwa miguu na Mwangi huku akitekeleza kitendo hicho cha ngono kwa punda huyo.
Maafisa hao wa polisi walipata mpira wa kondomu katika sehemu nyeti za punda huyo walipokuwa wanafanya uchunguzi kuhusu kesi hiyo.
Akijitetea mbele ya mahakama hiyo, Mwangi alieleza kuwa yeye ni kijana shupavu mwenye bidii na akaomba apewe kifungo cha miaka michache kwani ana uwezo wa kutegemewa siku zijazo kwa kuleta maendeleo katika jamii.
Mwangi alieleza kuwa hajawahi kushiriki kwa kutenda ouvu madai ambayo yalithibitishwa na mwendesha mashtaka Bi Cathrine Murugi aliyesema kwamba Mwangi hana historia ya kutotii sheria kwa kutenda maovu.
Hakimu Bi Juma alieleza kuwa amesikia tetesi zake Mwangi lakini Mahakama ilikuwa imempata na hatia ya kuhukumiwa.
Bi Juma alisema kwamba ni jambo la kushangaza kuwa visa vya watu kutenda maovu kama hayo kwa wanyama vinaendelea kuongezeka katika eneo hilo.
Hakimu huyo alisema kuwa wanaopatikana na hatia kama hiyo wanafaa kuadhibiwa vikali ili wawe funzo kwa wengine katika jamii.
“Umepatikana na hatia na kuhukumiwa miaka sita jela,”akasema Bi Juma.

No comments: