YALIYOJIRI TFF SIKU YA LEO
NYALLA,
NYAULINGO, NYENZI WASHINDA RUFANI
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Kamati
mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar es
Salaam.
Samwel
Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo
inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga
uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote
wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda
mbalimbali. Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya
Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya
kusikiliza hoja za Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na
kugundua yafuatayo; Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya
ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya
mgombea na ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho. Kamati
imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi
imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa
ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi. Kwa
vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa
mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona
itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile
tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote. Nyalla aliondolewa kwenye
uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza
kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1
kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya mgombea uongozi. Kwa upande wa
Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara
ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF,
Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo; Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea
sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa
Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi. Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo
kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake
kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi
nyingine za kitaifa. Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye
utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo,
Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na
amekidhi kigezo cha sifa za ugombea. Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa
miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha
ushiriki katika uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda
usiopungua miaka mitano. Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi
inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na
Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi. Kuhusu Ayubu Nyenzi
aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF
na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha
uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake
imesema; Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na
maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa
Kamati ya Uchaguzi. Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa
kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho
vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia
unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya
hivyo. Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na
kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika
nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu
unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na
Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6). Kwa kuzingatia hayo,
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi
anayogombea. Wakati huo huo, Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana
keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa
Kamati ya Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti
ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.
VITAMBULISHO KURIPOTI KOMBE LA DUNIA
VITAMBULISHO KURIPOTI KOMBE LA DUNIA
Maombi
ya vitambulisho kwa waandishi wa habari (Accreditation) wanaotaka kuripoti
Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil kwa Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yataanza kupokelewa kwa mtandao Desemba 7
mwaka huu kupitia akaunti ya FIFA Media Channel. Mwisho wa kupokea maombi
hayo itakuwa Januari 31 mwakani, hivyo kwa waandishi wanaotaka kupata
vitambulisho hivyo ni lazima wawe na akaunti ya FIFA Media Channel pamoja na
utambulisho wa mtumiaji wa akaunti hiyo (user ID). Kwa mujibu wa FIFA,
kila nchi itapewa idadi maalumu ya nafasi kwa waandishi (waandishi wa kawaida
pamoja na wapiga picha) baada ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia kumalizika
ambapo vigezo mbalimbali vitazingatiwa ikiwemo nchi kufuzu kwa fainali
hizo. Hivyo, nchi ambayo itakuwa imefuzu itakuwa na nafasi zaidi
kulinganisha na zile ambazo hazitakuwa na timu katika fainali hizo za
Brazil. Mgawanyo wa nafasi zitakazotolewa kwa Tanzania utapangwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kulingana na maombi
yatakayokuwa yamewasilishwa FIFA kupitia FIFA Media Channel. TFF inatoa
mwito kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu ambao hawana akaunti FIFA Media
Channel kuhakikisha wanakuwa nayo mapema ili waweze kutuma maombi yao.
SIMBA YAIVAA PRISONS, YANGA MGENI BUKOBA VPL
SIMBA YAIVAA PRISONS, YANGA MGENI BUKOBA VPL
Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya
nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na
Bukoba mkoani Kagera. Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa
ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons
inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo
wa ligi hiyo. Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa
ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi
yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting
inalazimika kuifunga Simba. Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake
iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja
dhidi ya Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao
kama ilivyo kwa wapinzani wao Tanzania Prisons. Viingilio katika mechi
hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi
zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa 4 kamili
asubuhi. Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja
wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson
Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage. Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa
tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya
kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika
nafasi ya nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na
moja. Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka
na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya
Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14. Mwamuzi
Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti United na
Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es
Salaam. Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13
mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini,
Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu
(Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu,
Turiani). Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia
TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi
katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu
itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.
FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII
FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII
Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu inaendelea wikiendi hii ambapo
kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT itakayochezwa
kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini
Iringa. Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini
mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa
kesho (Oktoba 12 mwaka huu). Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa
(Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa
kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad. Timu zote nane za kundi C
zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT
Kanembwa ya Kigoma. Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali
Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma
utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.
No comments:
Post a Comment