YALIYOJIRI TFF LEO
MSUMBIJI U 20 KUWASILI OKTOBA 25
Timu
ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inawasili nchini
kesho (Ijumaa, Oktoba 25 mwaka huu) saa 8.30 mchana tayari kwa mechi ya kwanza
ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania itakayofanyika Jumamosi
(Oktoba 26 mwaka huu).
Msumbiji
itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ndege ya LAM
ikiwa na msafara wa watu 25 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi. Timu
hiyo itafikia kwenye hoteli ya Sapphire iliyopo maeneo ya Gerezani, Dar es
Salaam.
Mara
baada ya kuwasili JNIA, kocha na nahodha wa timu hiyo watazungumza na waandishi
wa habari juu ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kwa
upande wa U20 chini ya Kocha Rogasian Kaijage imejiandaa vizuri kwa ajili ya
mechi hiyo, na kesho saa 10 jioni itafanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio
kwa mechi hiyo ni sh. 1,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya
chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati
VIP A itakuwa sh. 10,000.
Kamishna
wa mechi hiyo Evelyn Awuor kutoka Kenya tayari amewasili nchini wakati waamuzi
kutoka Burundi wanatarajia kuwasili leo saa 1 usiku kwa ndege ya Kenya Airways
wakiunganishia safari yao Nairobi, Kenya. Maofisa wote wa mechi hiyo wanafikia
hoteli ya New Africa.
UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA
Uchaguzi
wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) unafanyika
kesho (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee
Tower kuanzia saa 3 asubuhi.
Mgeni
rasmi katika mkutano huo wa Bodi ya TPL ambao unafanyika kwa mara ya kwanza
atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga.
Kwa
mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni
wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Viongozi
wa klabu za FDL wamefikia hoteli ya Royal Valentino iliyoko Barabara ya Uhuru
wakati wale wa VPL ambao pia watashiriki Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) wamefikia hoteli ya Landmark iliyopo Ubungo.
Wagombea
kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid
(Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib
Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.
No comments:
Post a Comment