Thursday, October 17, 2013

TANZANIA YAZIDI KUPOROMOKA VIWANGO VYA FIFA
SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetoa orodha mpya ya viwango vya ubora kwa mwezi huu huku Tanzania ikizidi kudidimia kwa kuporomoka kwa nafasi mbili.
Katika orodha hizo Tanzania imeshuka mpaka katika nafasi ya 129 kutoka nafasi ya 127 waliyokuwepo mwezi uliopita. Kwa upande wa Afrika Ivory Coast wameendelea kuongoza kwa kushika nafasi ya 17 katika orodha hizo duniani wakifuatiwa na Ghana ambao wanashika nafasi ya 23 huku Algeria nao wakiwa katika nafasi ya 32. Mabingwa wa Afrika Nigeria wanashika nafasi ya nne kwa kushika nafasi ya 33 na tano bora kwa upande wa Afrika inafungwa na Mali walioko katika nafasi ya 41. Mabingwa wa dunia Hispania wameendelea kubaki katika nafasi ya kwanza kwenye orodha hizo wakifuatiwa na Ujerumani waliopanda mpaka nafasi ya pili na kuiondoa Argentina iliyopo katika nafasi ya tatu. Nafasi ya nne katika orodha hizo inashikiliwa na Colombia ambao wamepanda kwa nafasi moja kulinganisha na walipokuwa mwezi uliopita huku Ubelgiji wakifunga tano ya orodha hizo.

SABA BORA KATIKA ORODHA ZA FIFA KUONGOZA DROO ZA UPANGAJI RATIBA YA KOMBE LA DUNIA BRAZIL.

SWITZERLAND itakuwa mojawapo ya nchi nane zitakazoongoza droo ya ratiba ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 itakayofanyika Desemba mwaka huu baada ya kukwea mpaka nafasi ya saba katika orodha za ubora dunia zilizotangazwa leo. Hispania, Argentina, Ujerumani, Colombia, Ubelgiji na wenyeji Brazil nao pia wataongoza droo hiyo wakiungana na Uruguay kama wakifanikiwa kuwafunga Jordan katika mechi za mikondo miwili za mtoano mwezi ujao. Kama Uruguay ikishindwa kufuzu michuano hiyo, Uholanzi ambao wanashika nafasi ya nane katika orodha hizo sambamba na Italia itachukua nafasi hiyo. Katika kanuni za Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Brazil ukijumlisha na timu saba zilizopo katika orodha za juu za shirikisho hilo ndio zitaongoza droo ya upangaji ratiba ya michuano hiyo.

No comments: