Wednesday, October 9, 2013

MBUNGE NCHINI KENYA AWAZAWADIA WANAWAKE 16 KWA KUJIFUNGUA WATOTO
Mimba
WANAWAKE 16 katika eneo la Kirinyaga huko nchini kenya wametuzwa na mbunge wao wa Gichugu Bw Ejidio Njogu Barua baada ya kujifungua watoto.
Mbunge huyo aliwasifu wanawake hao kwa kutilia mkazo wito wake kuwa waimarishe juhudi zao za kuongeza kizazi katika maeneo hayo na akaahidi kuendelea mbele na mradi huo.
Katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Kanisa la Katoliki Mururi katika eneo la bunge hilo mnamo Ijumaa, kila mwanamke alipokea Sh500, wote wakipata jumla ya Sh 8,000.
“Nilikuwa nimepata habari za kufurahisha kuwa ni wanawake 48 ambao walikuwa wajitokeze mahali hapa. Nilikuwa nimebeba Sh24,000 lakini nimeshangaa kupata wanawake 16 pekee. Lakini silalamiki sana kwa kuwa hii ni idadi nzuri ikizingatiwa kuna miezi kadhaa ambayo haungemuona mja mzito barabara za eneo hili letu,” akasema.
Bw Barua alisema kuwa atazidisha kampeni yake miongoni mwa vijana ambao wamekwama katika unywaji wa pombe kiholela na kisha kusahau majukumu yao ya kijamii warekebike na kisha waanzishe familia zao.
“Mimi nataka kuwatangazia kwamba juhudi hizi zitakuwa zikiendelea kila wikiendi ambapo ukishapata mimba na kisha ujifungue mtoto, nitakutuza
Sh500 kama zawadi. Kisha tufuatilie juhudi hizo kwa kuhakikisha umejiunga na kikundi cha ustawi na upate hela za kujiendeleza kiriziki,” akasema.
Mradi huo ni sawia na mwingine unaoendeshwa na Gavana wa Kaunti hiyo Bw Joseph Ndathi ambaye pia huwatuza kina mama waliojifungua baada ya kuolewa na vijana ambao wamehepa ulevi.
Aliwahimiza viongozi wa kanisa wazindue maombi maalum ili vijana wa eneo hilo watilie mkazo uzazi.
Mbunge huyo alisema hali ya sasa kwa vijana ni kulewa pombe haramu na kisha kujisahau kifamilia.
 “Hatutaki kujiona kwa vyombo vya habari tukitangaziwa kwa wanawake wetu wanaandamana wakiwalaumu waume zao wakibugia pombe hatari,”akasema.
Mbunge huyo aliwachangamsha aliposema kuwa alikuwa akihofia kama atafanikiwa kuchaguliwa tena 2017 ikiwa vijana wa eneo hilo watasombwa na ulevi jinsi ilivyo kwa sasa na kisha kuaga dunia.
Alisema kuwa amekuwa akizuru hospitali ya Kianyaga na kuthibitisha kuwa wadi za kujifungulia wamama zimefanywa stoo za kuweka vifaa.
"Hii ni kwa sababu madaktari wamechoka kungoja waja wazito. Ni nadra sana wapate wanawake vijana wakiletwa humo wakiwa waja wazito,".
Bwana Barua alisema kuwa, kungekuwa na uwezekano wa kuunda sheria ya kuwashinikiza vijana waunde familia kwa lazima, angewasilisha mswada bungeni.
Aliomba waumini wajifunge kula na kunywa ili wamuombe Maulana kuwaokoa vijana. Aliapa kuwasukuma maafisa wa utawala kupambana na wagema wa pombe haramu.
Aidha, aliwataka wenyeji kuwashinikiza vijana wauteme ulevi na kisha waoe.
"Hata ikiwa itahitaji tuwahonge vijana hao ndio warekebike, tutawahonga," akasema.
 
Swahili hub

No comments: