ZAIDI YA WASICHANA 55,000 WATIMULIWA KWA MIMBA
Watoto wa kike zaidi ya
55,000 Tanzania Bara, walifukuzwa shule na kutengwa na jamii, baada ya
kupata mimba wakiwa shuleni katika kipindi cha muongo mmoja uliopita,
hatua iliyowaharibia kwa kiasi kikubwa ndoto zao za baadaye.
Kituo kinachotetea haki ya uzazi, kijulikanacho kama Center For
Reproductive Right cha Marekani, kimebaini hayo kutokana na utafiti wake
uliofanyika mikoa mbalimbali mwaka 2012/13. Mkurugenzi Mkazi wa kituo hicho Afrika, Evelyne Opondo alisema jana Dar es Salaam kwamba utafiti huo, ulilenga pia kubaini madhara yatokanayo na upimaji wa mimba kwa lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Opondo alisema imebainika zaidi ya asilimia 44 ya wasichana Tanzania Bara, ama wamejifungua au kupata mimba wakiwa na umri wa miaka 19 na wengi kati yao walitengwa na jamii.
Ripoti ya utafiti huo uliozihusisha shule za kutwa na za bweni za serikali, binafsi na dini, ilieleza kuwa ingawa hakuna sheria, sera au miongozo inayoruhusu upimaji wa mimba kwa lazima , lakini wakuu wa shule na viongozi wa serikali za mitaa wamekuwa wakifanya vitendo hivyo wakidhani kwamba vinaruhusiwa.
No comments:
Post a Comment