Monday, September 9, 2013



MWANAMKE MBABE  ALIYEJARIBU KUMPA SUMU MUMEWE ILI AFE, AENDA JELA MIAKA MITATU.
Bw Charles Mbaruku Kimani
MWANAMKE mmoja amefungwa jela miaka mitatu na mahakama ya Murang’a kwa kujaribu kumpa sumu mumewe na kumpiga.
Bi Purity Wanjiku Mbaruku, 30, ambaye ni mama wa watoto wanne alishtakiwa kwa makosa mawili mbele ya Hakimu Mkuu mkazi Bw Joseph Masiga.
Katika shtaka la kwanza, Bi Wanjiku alishtakiwa kuwa mnamo Agosti 24 mwaka huu katika kijiji cha Matongu, lokesheni ya Kimathi eneo la Kiharu, alijaribu kumpa sumu mumewe Bw Charles Mbaruku Kimani.Vile vile alishtakiwa kwa kumpiga na kumjeruhi mumewe.
Katika shtaka la kwanza, kiongozi wa mashtaka Bw Paul Gathara alieleza mahakama kuwa mshtakiwa alimkaba koo mumewe na kujaribu kumnywesha dawa ya kuua kupe aina ya ‘Tria-Tix’ saa nne na nusu usiku.
Alielezea mahakama kuwa Bi Wanjiku alikusudia kumwua Bw Kimani kwa kumpa sumu hiyo hatari.
“Hata hivyo mlalamishi alimuuma mshtakiwa mkono na akapiga yowe  na majirani wakaja,” alisema Bw Gathara Ijumaa.
Mahakama ilielezwa kwamba Bw Kimani,54, alitoa ripoti katika kituo cha polisi cha Kabuta mara moja na kutumwa katika kituo kikuu cha polisi Murang’a mjini na kisha baadaye kwenda hospitali kuu ya Murang’a ambapo alitibiwa.
Baada ya kuandikisha ripoti, alipewa fomu ya polisi ya P3 kuonyesha kwamba alipata majeraha na polisi wakamkamata mkewe hapo siku ya Alhamisi.
Akijitetea, mwanamke huyo wa umri wa miaka 30 alisema walikuwa wakizozana kwa miaka mingi tangu aolewe na Bw Kimani miaka 13 iliyopita na amepata ugonjwa wa shinikizo la damu kufuatia ugomvi wa kila saa.
“Yeye ndiye aliyetaka kunipa sumu na amefanya tuzozane kwa miaka mingi mpaka nikapata ugonjwa wa shindikizo la damu,” aliambia mahakama.
Lakini hakimu Masiga alisema kosa hilo ni kubwa mno kwani lingepelekea kifo cha mlalamishi akiongeza mshtakiwa alifaa kupata adhabu kali.
Alimfunga miaka miwili kwa kosa la kwanza na mwaka mmoja kwa shtaka la pili.
 Bw Kimani alifurahia uamuzi wa mahakama na kusema ataenda katika afisi inayosimamia maswala ya watoto na kudai wanawe wawili aliozaa na mkewe ambao wanaishi na nyanya yao huko Kaunti ya Kirinyaga.
Vile Vile aliandikisha ripoti katika kituo cha polisi cha Murang’a akidai amepokea vitisho kutoka kwa shemeji yake mmoja kwa njia ya simu.
“Nilipigiwa simu na ndugu mmoja wa bibi yangu ambaye anaishi Kimicha kaunti ya Kirinyaga na akanionya kuwa nitakiona cha mtema kuni kwa kumshtaki dadake,” aliambia polisi mnamo Alhami.
Swahili hub

No comments: