TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO
USAJILI
WA WACHEZAJI HATUA YA KWANZA WAMALIZIKA
Hatua ya
kwanza ya usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2013/2014 imefungwa rasmi jana
(Agosti 5 mwaka huu) ambapo klabu zote za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zimewasilisha
usajili wa vikosi vyao ndani ya wakati.
Baadhi ya
klabu zimefanya makosa madogo madogo katika usajili ambapo zimepewa siku ya leo
(Agosti 6 mwaka huu) kufanyia marekebisho kasoro hizo. Hivyo kesho (Agosti 7
mwaka huu) majina ya vikosi vyote yatabandikwa kwenye mbao za matangazo za
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kipindi cha pingamizi
kitakachomalizika Agosti 12 mwaka huu.
Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa itakutana
Agosti 13 na 14 mwaka huu kupitia na kufanyia uamuzi usajili wa wachezaji wenye
matatizo. Hatua ya pili ya usajili itaanza tena Agosti 14 mwaka huu
ikihusisha wachezaji ambao watakuwa hawajasajiliwa katika Ligi Kuu ya Vodacom
msimu huu na wale kutoka nje ya Tanzania. Hivyo, dirisha la uhamisho kwa
wachezaji wa kimataifa litafungwa baada ya hatua ya pili ya usajili kumalizika
Agosti 29 mwaka huu.
Timu ya 3Pillars Football Club ya Nigeria sasa inaruhusiwa kucheza mechi za kirafiki nchini baada ya kupata idhini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Nigeria (NFF). Awali ilikataliwa kucheza mechi za kirafiki nchini kwa vile haikuwa na barua kutoka NFF, lakini sasa Shirikisho hilo limetoa idhini hiyo. Pia ziara yake haikuwa inaratibiwa na wakala wa mechi anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) au mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment