Saturday, August 31, 2013

MWANAUME ADAI MKEWE ALITAKA KUMNYWESHA SUMU ILI AFE HUKO NCHINI KENYA
Bw Charles Mbaruku Kimani
Swala la unyanyasaji dhidi ya wanaume nchini Kenya unaendelea kushika kasi baada ya mwanamume  mmoja kunusurika kifo baada ya mkewe kumlazimisha kunywa sumu.
Bw Charles Mbaruku Kimani kutoka kijiji cha Matongu kata ya Kimathi eneo la Kiharu alidai mkewe alimpiga dafrau usiku na kutaka kumnywesha sumu kwa nguvu lakini akakataa.
Akiongea  katika kituo cha polisi mjini Murang’a ambapo aliandikisha ripoti, jamaa huyo wa miaka 54 alidai mkewe ana mazoea ya kumshambulia akishirikiana na mwanawe wa kiume.
Bw Kimani alisema wameoana kwa miaka 13 na wamekuwa wakizozana kwa siku nyingi huku mkewe akitoroka kwa wazazi wake mara kadhaa katika kijiji cha Kimicha.
Alisema kuwa siku ya Jumamosi usiku, mkewe alichanganya dawa ya kuua kupe na kuitia kwenye chupa na kumkaba koo mzee huyo huku akitaka anywe dawa hiyo ili afe.
“Tulikuwa tumetoka safari na ndani ya nyumba kulikuwa na giza kwani hatukuwa tumewasha taa na nilikuwa nimeketi  kitini wakati mke wangu aliponishambulia,” alisema Bw Kimani ambaye alitibiwa hospitali kuu ya Murang’a baada ya kisa hicho.
Mwanamme huyo ambaye anafanya biashara ya kuuza changarawe alidai mkewe alimshika kwenye sehemu ya shingo na kuelekeza chupa hiyo iliyojaa sumu kwenye mdomo wake lakini mwanamme huyo akamuuma mkewe mkono wakati wa kisa hicho.
Hata hivyo, kiasi kidogo cha sumu kiliingia mdomoni na akalazimika kukimbizwa hospitali ili kuzuia maafa zaidi.
Sehemu ya mdomo ilionekana ikiwa imechomwa na dawa hiyo huku akiongezea alianza kuumwa na tumbo baada ya kutiwa sumu hiyo mdomoni.
“Nilipomuuma mke wangu mkono,alipiga mayowe na majirani wakafika na kunipa maji nikabugia mdomoni ili nisife,” alisema Bw Kimani.
Alisema ameandikisha ripoti katika kituo cha polisi cha Murang’a huku akiongeza mkewe alitorokea kwao nyumbani Kirinyaga na baadhi ya mali yake.
Mwanamme huyo alisema alimwoa mkewe akiwa na watoto wawili na hapo baadaye wakazaa wengine wawili.
Hata hivyo alisema mkewe na mwanawe mmoja wa kiume wamekuwa na mazoea ya kumashambulia na kusambaratisha biashara yake ya duka
Aliongezea kuwa anahofia usalama wake kwani anashuku mkewe anaweza panga njama ya kumuua.

Swahili hub

No comments: