Tuesday, August 13, 2013

MWANAMKE ATEKETEZA NYUMBA KWA MOTO BAADA YA MUME KUOA MKE WA PILI
Mji wa Migori
Baada ya mwanamume mmoja kutoka mji wa Migori nchini Kenya kumuoa mke wa pili mwishoni mwa wiki ilimsababishia hasara ya mamilioni baada ya mke wa kwanza kukasirika na kuteketeza nyumba yake. 
Mkewe aliyejawa na hasira alirushia nyumba hiyo bomu la petroli katika kijiji cha Nyakona,  Got Kachola,  eneo bunge la Nyatike kupinga ndoa hiyo.
Mali zote zilizokuwa katika nyumba hiyo ikiwa ni pamoja na nguo, samani na vyombo vya elektroniki vya thamani ya Sh1 milioni alivyomiliki Bw Simeon Osewe, viliteketea kabisa.
Mkewe wa kwanza, aliye mama wa watoto wawili aliwasili kwa siri kutoka Nairobi anakofanya kazi na kumshambulia mke mwenza aliyekuwa akilala katika nyumba hiyo.
“Nilikuwa mjini Migori kwa shughuli za kibinafsi nilipopigiwa simu nikiarifiwa kwamba nyumba yangu ilikuwa ikichomeka. Mke wangu wa pili alifanikiwa kutoroka na kumwacha mke wa kwanza aliyechoma nyumba hiyo,” akasema Bw Osewe.
Juhudi za wanakijiji kuzima moto huo hazikufaulu na moto mkali ukateketeza nyumba hiyo hadi kila kitu kikawa jivu.
Mkuu wa polisi wa Nyatike  Bw Richard Mukwate alisema mwanamke huyo alikamatwa akijaribu kutoroka eneo la mkasa.
Alisema mwamamke huyo alionekana kukasirishwa na hatua ya mumewe kuoa mke wa pili na kuishi katika nyumba hiyo.
“Tumemzuia katika kituo cha polisi cha Macalder na tutamfikisha mahakamani wiki hii na kumfungulia mashtaka ya kuchoma mali,” akasema Bw Mukwate.
Bw Osewe alisema aliamua kuoa mke wa pili baada ya mke wa kwanza kukataa kuishi naye mashambani.
“Mwanamke huyo alikataa wito wangu wa kuja nyumbani akisema anapenda mazingira ya Nairobi na hii ikanifanya kuoa kwa sababu sikuweza kuishi peke yangu mashambani,” akasema.
Swahili hub

No comments: