Bi Faith Wairimu Maina akiwa mahakamani Nairobi Juni 19, 2013.
Mwanamke mmoja leo amekiri kortini Nairobi kwamba alikuwa amepanga kulipa watu Sh200,000 wamuue mumewe.
Faith Wairimu Maina,40, mkazi wa mtaa wa Zimmermann, Nairobi aliyekuwa na hasira za mkizi aliapa atamuua mumewe Bw John Muthee Guama kwa sababu alikuwa atoi huduma nyumbani.
“Mimi sijui kule anakopeleka pesa zake.Kila siku ni mimi nanunulia watoto chakula na kugharamia mahitaji ya nyumbani. Pesa anazopata mume wangu ni za kulewa na kustarehesha wanawake wengine,” Wairimu alimweleza hakimu mwanadamizi Bi Peter Ndwiga.
Akiendelea na kujitetea alisema, “ Nimekuwa na taabu chungu nzima. Mimi na watoto wawili wangu tumetaabika vya kutosha huku mume wangu akiendelea na maisha ya raha mstarehe.”
Alisema kwamba ni yeye huwalipia watoto karo kwa vile “mumewe amewatupa.”
Ili kufanikisha njama yake aliwakodi watu watatu wa kumuua mumewe na kuahidi kuwa angewalipa Sh200,000 bila kujua kwamba walikuwa maafisa watatu wa polisi.
Waliwasiliana naye na akakubali kuwalipa malipo ya papo hapo ya Sh40,000 na makubaliano yakawa walipwe masalio baada ya kufikisha kwake mavazi ya mumewe yakiwa na damu.
Polisi hao waliwasiliana na mumewe mwanamke huyo, Muthee, na wakachukua mavazi yake na kuyalowesha damu kutoka kwa kichinjio na kuchanganya na damu ya matumbo.
Ushahidi huo uliwasilishwa kortini.
Kutiwa nguvuni kwa Wairimu Juni 17 kulimshtua alipogundua wanaume watatu aliopanga nao kwamba angewalipa Sh200,000 kumuua mumewe ndipo arithi mali yake, walikuwa maafisa wa polisi kutoka kitengo cha Flying Squad.
Bw Ndwiga alifahamishwa Wairimu aliota mpango huo wa kumuua mumewe baada ya kugundua alikuwa na mwingine kwa jina Njeri Wambaa.
Hakimu Mkuu Peter Ndwiga ameamua mwanamke huyo arudishwe rumande gereza la wanawake la Langata akisubiri kuhukumiwa Juni 2.
|
No comments:
Post a Comment