ANAYETUHUMIWA
KULAWITI, KUNAJISI NA KUWATOBOA MACHO WATOTO AKAMATWA
MTUHUMIWA sugu wa matukio ya unajisi na vitendo vya
kikatili dhidi ya watoto, anashikiliwa na Polisi mkoani Shinyanga, baada ya
kukurupushwa katika jaribio la kutaka kumnajisi na kumtoboa macho mwanafunzi
mwenye umri wa miaka minane.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist
Mangala alisema ofisini kwake jana, kuwa mtuhumiwa huyo, Jacob Mayani (28),
ameshanajisi watoto wanne wa umri wa kati ya miaka minane hadi 10 na kuwatoboa
macho.
‘’Mayani anatuhumiwa kunajisi na kufanyia ukatili wa
kutoboa macho watoto wanne wenye umri wa kati ya miaka nane hadi 10, kwa lengo
la kutaka kuvuruga ushahidi ili wasimtambue,’’ alidai Kamanda Mangala.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Mangala, mtuhumiwa
alikamatwa mwishoni mwa wiki kwenye shamba la mahindi katika mtaa wa Mwasele
manispaa ya Shinyanga, baada ya jaribio lake la kutaka kumnajisi mtoto mmoja
kushindwa.
Inadaiwa jaribio hilo lilishindwa baada ya mtoto
aliyekusudiwa kunajisiwa, kufanikiwa kuponyoka mikononi mwa mtuhumiwa na
kutimua mbio huku akipiga kelele za kuomba msaada. Kutokana na kelele hizo,
Kamanda Mangala alisema wasamaria wema walijitokeza wakamkamata mtuhumiwa na
kumfikisha kituo cha Polisi.
Kamanda Mangala alisema mtuhumiwa alifanya unyama
huo katika muda usiozidi mwezi mmoja katika matukio na maeneo tofauti ya
Kitangili, Ndembezi na Ndala.
Alisema watoto wawili kati yao, walilazwa katika
Hospitali ya Rufaa ya Bugando na mmoja hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Kwa
mujibu wa madai hayo, madaktari walitoa taarifa Polisi kwamba jicho la mmoja wa
watoto hao limeharibika baada ya kutobolewa.
Kamanda Mangala alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa
huyo jana, watoto wawili waliopata kufanyiwa unyama huo, walifika kwenye kituo
cha Polisi mjini hapa na kumtambua mtuhumiwa kwenye gwaride la utambulisho.
Alisema mtuhumiwa ni mkazi wa mshikamano katika
manispaa ya Shinyanga na hujishughulisha na kazi ya kutoa huduma ya usafiri wa
baiskeli, maarufu kwa jina la bodaboda na uuzaji wa urembo.
Inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akirubuni watoto hao kwa
kuwapa mahindi mabichi ya kuchoma na mavazi ya kubana au vipodozi vya urembo.
Kamanda wa Polisi alisema kutokana na tabia na
mwenendo wa mtuhumiwa, inahofiwa kuna watoto wengi waliofanyiwa vitendo hivyo,
lakini kwa sababu moja au nyingine wazazi au watoto hawajaripoti matukio hayo.
Kamanda huyo alitoa mwito kwa wazazi na walezi,
kutoa taarifa kama watoto wao walinajisiwa na mtuhumiwa. Mtuhumiwa anashikiliwa
na Polisi na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa mahakamani kujibu
mashitaka yanayomkabili.
Chanzo:
Habarileo

No comments:
Post a Comment