MGANGA WA JADI MIAKA 86 AMBAKA MTOTO WA MIAKA 6
![]() |
| Ndumba Nangaye |
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida iliyowashangaza wengi mganga wa kienyeji, Edward Mwakalebela (86), anadaiwa kumbaka mtoto wa miaka 6.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Sioni Ijuni, amesema kuwa mganga huyo mkazi wa kijiji cha Ndwanga, kata ya Katumbasongwe, wilayani Kyela, mkoani Mbeya, alitenda kosa hilo Aprili 20 mwaka huu majira ya saa 8 usiku.
Alisema aligundua tukio hilo baada ya mtoto wake kulalamika kusikia maumivu ya tumbo naye kumpa huduma ya kwanza kwa kumkanda na maji ya moto lakini baadaye aliona damu zikimtoka sehemu za siri.
Alisema alipomhoji zaidi ndipo mtoto huyo alipomtaja babu huyo ambaye ni jirani yake kuwa alimwingilia kimwili kwa kumfanyia kitendo hicho cha kinyama.
Kutokana na hali hiyo mama huyo alisema aliamua kupeleka taarifa hiyo kwa mwenyekiti wa kijiji akiwa na mumewe Kifoji Mwabusila na baada ya mwenyekiti kuandika maelezo yao aliwaamuru kwenda polisi ili wapatiwe kibali cha kwenda kutibiwa nao wakafanya hivyo kisha baadaye polisi walimkamata mtuhumiwa na kumtia mbaroni.
“Tulipokuwa kwa mwenyekiti wa kijiji, babu huyo alikiri kutenda kosa hilo na aliomba msamaha akidai ni shetani tu alimpitia huku akiomba mambo hayo yamalizwe kimya kimya bila kwenda polisi jambo ambalo lilikuwa gumu kwetu,” alisema mama mzazi wa mtoto huyo.
Alieleza kusikitishwa na tukio hilo ikizingatiwa kuwa mzee huyo ni jirani yake na amekuwa na mazoea ya kumtuma mtoto wake kama mjukuu wake lakini kumbe alikuwa anatengeneza mazingira ya kumfanyia unyama huo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dickson Mwakasinga, alikiri kuwepo na tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kupelekewa taarifa ya uwepo wa tukio hilo alifuata taratibu zote na kumkabidhi mtuhumiwa huyo mikononi mwa polisi wilaya kwa hatua zaidi za kisheria.
Mganga wa zamu aliyemtibu mtoto huyo, Tabu Mwakalundwa, alikiri kumpokea mgonjwa huyo na kudai kuwa aliingiliwa na kuharibiwa vibaya na kwamba wanafanya jitihada za haraka za kumtibu mtoto huyo ili arudi katika hali yake ya kawaida.
Nao wananchi wa kijiji hicho wamelihusisha tukio hilo na imani za kishirikina kwa kuwa mzee huyo ni mganga wa kienyeji na kuwa umri alionao na kitendo alichomfanyia mtoto huyo ni kinyume na maadili ya Mtanzania.
Tanzania daima

No comments:
Post a Comment