Thursday, March 14, 2013

TANZANIA YAPANDA KWA NAFASI NANE KATIKA VIWANGO VYA FIFA 

SHIRIKISHO la Soka Dunia-FIFA limetoa viwango vipya vya ubora katika soka kwa mwezi huu ambapo Tanzania imekwea kwa nafasi nane mpaka katika nafasi ya 119 kwenye viwango hivyo. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 127 baada ya kuporomoka kwa nafasi tatu ukilinganisha na viwango vya mwezi Januari ambapo ilikuwa katika nafasi ya 124 baada ya kupanda kwa nafasi sita. Kwa upande wa nchi zinazoshika tano bora duniani kwenye orodha hizo zote zimeendelea kubakia katika nafasi zao ambapo Hispania imeendelea kuongoza ikifuatiwa na Ujerumani katika nafasi ya pili huku katika nafasi ya tatu ikishikwa Argentina wakati Uingereza na Italia zinashika nafasi ya nne na tano. Kwa upande Afrika Ivory Coast wameendelea kung’ang’ania katika nafasi ya kwanza baada ya kuporomoka kwa nafasi moja mpaka ya 13 duniani wakifuatiwa na Ghana ambao wako katika nafasi ya 20 huku Mali nao wakiwa hawako mbali baada ya kupanda nafasi moja mpaka ya 24. Mabingwa wa Afrika Nigeria wao wako katika nafasi ya nne kwa upande wa Afrika baada ya kubakia katika nafasi yao ya 30 kama ilivyokuwa mwezi uliopita kwenye orodha za dunia huku tano bora kwa upande Afrika ikifungwa na Algeria.

No comments: