TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF

TFF BADO YASISITIZA
KUMUONA WAZIRIMUKANGARA.
RAIS
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara kwa
kukubali ombi la Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa mazungumzo na kumsihi
asitishe hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo kikao hicho
kitakapofanyika. Waziri Mukangara ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa
marekebisho ya katiba ifikapo tarehe 15 Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi
ifikapo tarehe 25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe
limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11,
2013). Katika barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko
nje ya nchi, Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi
2013 kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na
Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana na
Naibu Katibu Mkuu. Katika barua hiyo pepe, Rais Tenga ameeleza madhumuni
ya kutaka kuonana na Waziri Mukangara kuwa ni kwanza “kukushukuru kwa kukubali
kuonana na ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw.
Alex Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, tarehe 6
Machi 2013. “Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19
Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako. “Kukuarifu kuwa nimepokea
maagizo yako uliyoyatoa kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa
njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua
hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo
uliyoyatoa.” Tenga, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda
Marrakech, Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF
ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya uchaguzi
wa rais.
KAIJAGE KOCHA MPYA TWIGA
STARS
ROGASIAN
Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya
wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface Mkwasa
kujiuzulu katikati ya mwaka jana. Mkwasa, ambaye alikuwa nyota wa Yanga na
Taifa Stars, alijiengua kufundisha timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada
ya Twiga Stars kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza
fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial
Guinea. Twiga ilipata bao muhimu la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa
na wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema
bao la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo
wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali
hizo. Kaijage ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots)
pamoja na programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na
Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga Stars kwa
mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam. Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden),
Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther Chabruma
(Sayari), Esther Mayalla (TSC Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo
(Mbarahati Queens), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa (Sayari) na
Fatuma Omari (Sayari). Flora Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh
Academy), Hellen Maduka (Bujora), Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC
Academy), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba
(Mburahati Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa
(Sayari). Nabila Ahmed (Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar),
Pulkeria Charaji (Sayari), Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite),
Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor,
Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena
Khamis (Mburahati Queens).
YANGA, TOTO AFRICANS
KUUMANA DAR
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea
kesho (Machi 9 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa wenyeji
wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi wa mechi hiyo namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa
na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni Salim
Singano kutoka Tanga wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza. Nayo
Polisi Morogoro itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na nyingine mbili
zinazofuata itakuwa bila kocha wake Steward John Hall ambaye Kamati ya Ligi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu. Charles
Komba kutoka Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136
itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani. Ligi hiyo
itaendelea tena keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya Tanga. Waamuzi wa
mechi hiyo ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse Erasmo na Vicent Mlabu wote
kutoka Morogoro.
RHINO, KANEMBWA ZASAKA
TIKETI VPL
KINDUMBWENDUMBWE cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9
mwaka huu) katika makundi yote matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa
mpira wa miguu yakiwa kwenye mechi za Rhino Rangers ya Tabora na Kanembwa JKT
ya Kigoma. Timu hizo ndizo ziko katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya
kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari
Mbeya City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar es Salaam zimeshapata tiketi za
kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na B.
Rhino Rangers itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora, wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza. Mechi nyingine za kundi C ni Mwadui vs Polisi Tabora
(Kambarage, Shinyanga), na Morani vs Polisi Mara (Kiteto, Manyara). Mechi za
kundi A ni Majimaji vs JKT Mlale (Majimaji, Songea), Mkamba Rangers vs Mbeya
City (Sokoine, Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso (Samora,
Iringa). Mshikeshike ya kundi B ni Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda
Sijaona, Mtwara), Villa Squad vs Green Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi
Dar vs Transit Camp (Mabatini, Mlandizi) wakati Tessema na Moro United
zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment