Wednesday, March 6, 2013

LIGI KUU TANZANIA BARA, MTIBWA SUGAR YAZIPUMULIA SIMBA SC NA COASTAL BAADA YA KUIFUNGA MGAMBO MKWAKWANI LEO

 


MTIBWA Sugar ya Morogoro imeendeleza makali yake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jioni ya leo kuitandika Mgambo Shooting bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Shujaa wa Mtibwa jioni ya leo alikuwa yule yule beki aliyewafungia Wakata Miwa hao wa Manungu bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Simba SC, Salvatory Ntebe, ambaye leo alifunga dakika ya 89.
Kwa ushindi huo, Mtibwa inayobaki nafasi ya tano imefikisha pointi 31, baada ya kucheza mechi 20, hivyo kulingana kwa pointi na Coastal Union ya Tanga iliyo nafasi ya nne na mabingwa watetezi Simba SC waliopo katika nafasi ya tatu, ambazo zina wastani mzuri wa mabao. 
Hali imezidi kuwa mbaya kwa African Lyon baada ya kuchapwa bao 1-0 na Ruvu Shooting jioni ya leo, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Bao lililoizamisha Lyon leo lilifungwa na Abdulrahman Mussa dakika ya 29. Lyon sasa inaendelea kushika mkia katika Ligi Kuu, kwa kubaki na pointi zake 13, baada ya kucheza mechi 20.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo leo, JKT Oljoro imeichapa Tazania Prisons 1-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, bao pekee la Paul Nonga dakika ya 60.
bongostaz.blogspot.com

No comments: