Tuesday, January 22, 2013

SARE ZAENDELEA KUTAWALA MICHUANO YA AFCON 2013


Nigeria yatoka sare na Burkina Faso 1-1
Zambia nayo yavutwa shati na Ethiopia ya 1-1

Wachezaji wa Nigeria wakisherekea bao lao
 Nigeria imeanza kampeini yake ya kinyang'anyiro cha kuwania kombe la Mataifa ya Afrika, nchini Afrika Kusini kwa kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na Burkina Faso katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi C.

Nigeria ilipata bao hilo muhimu na la ushindi kupitia kwa mshambuliaji wake Emmanuel Emenike, anayeichezea klabu ya Spartak Moscow ya Urussi kunako dakika ya 23.

Kikosi hicho cha Super Eagles, kilifanya mashambulizi kadhaa katika lango la Burkina Faso, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Baada ya dakika za kwanza 45, zilimalizika huku Nigeria ikiwa kifua mbele kwa bao moja kwa bila.

Matumaini ya kocha wa Super Eagles, Stephen Keshi, ambaye anaiongoza timu kwa mara ya kwanza katika fainali hizo ya kuandikisha ushindi wake wa kwanza ulitumbukia nyongo pale Burkina Faso iliposawazisha katika dakika za ziada.

Katika mechi ya awali, Mabingwa watatezi wa kombe la mataifa ya Afrika Chipolopolo ya Zambia wameanza kampeini ya kutetea kombe hilo waliloshinda mwaka uliopita kwa kutoka sare ya kufungana bao moja kwa moja na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya Kundi C nchini Afrika Kusini.

Kinyume na matarajio ya wengi Ethiopia ilionyesha mchezo mzuri wakati wa mechi hiyo na mara nyingi wachezaji wake wakionekana kuwathibiti wachezaji wa Chipolopolo.

Kwa mara nyingine tena timu hiyo ya Zambia, imeonyesha kuwa kwa sasa haiko katika hali nzuri kama ilivyokuwa mwaka uliopita.

Wakati wa mechi hiyo beki wake Chisamba Lungu alimuangusha mshambulizi wa Ethiopia Saladin Seid, kwenye eneo la hatari na bila kusita refa wa mechi hiyo akatoa adhabu ya penalti.

Lakini kipa wa Zambia Kennedy Mweene aliokoa mkwaju uliopigwa na Seid na hivyoi kufufua matumaini ya mabingwa hao watatezi.

Dakika chache baadaye, kipa wa Ethiopia, Jemal Tassew alipewa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Chisamba Lungu.

Licha ya kuwa alikuwa akiondolewa uwanjani kwa machela refa wa mechi hiyo alimpa kipa huyo kadi nyekundu kutokana na mchezo mbaya na hatari aliouonyesha.

Dakika chache baada ya tukio hilo mabingwa hao watetezi wakafunga bao lao la kwanza kupitia kwa mchezaji Collins Mbesuma kunako dakika ya 45 kipindi cha kwanza.

Katika kipindi cha pili licha ya kucheza wachezaji kumi pekee kwa muda mrefu, Ethiopia ilisawazisha kunako dakika ya 65 kupitia kwa mchezaji Adane Girma.

Ithiopia ilithibiti mpira wa asilimia kubwa katika kipindi cha pili na hivyo kuzima matumaini ya mabingwa hao watatezi.

Mechi hiyo ilimalizika huku timu hizo mbili zikitoshana nguvu ya kufungana bao moja kwa moja.

Timu zote katika kundi hilo, Ethiopia, Burkina Faso, Nigeria na Zambia sasa zina alama moja kila mmoja.
Nigeria sasa itachuana na Zambia katika mechi yao ijayo kisha icheza na Ethiopia mechi yao ya mwisho ya makundi.


Burkina Faso nayo itacheza na Ethiopia mechi ijayo kisha ikamilishe kampeinin yake ya raundi ya kwanza na Zambia

KATIKA MECHI ZA LEO

IVORY COAST INAJIANDAA KUANZA KAMPEINI YAKE DHIDI YA TOGO.

TUNISIA NAYO INAJIANDAA KUCHUANA NA ALGERIA KATIKA MECHI NYINGINE KALI YA KUNDI D.

No comments: