Monday, January 21, 2013

SAJUKI, WASTARA KATIKA MAANA HALISI YA MAPENZI, TUJIFUNZE
SEHEMU YA MWISHO



Marafiki waaminifu wachache, hubaki na rafiki aliyepatwa na majanga. Hata hivyo, nao wanaweza kukimbia pale ambapo matatizo yanazidi. Marehemu Juma Issa Kilowoko ‘Sajuki’ na Wastara Juma Issa, hawakutupana, walishikamana mpaka kifo kimewatenganisha.

Kama Sajuki alivyofumba macho, akasisitiza Wastara ndiye mke wake pamoja na ulemavu aliopata mrembo huyo wakati wanakaribia kufunga ndoa, vivyo hivyo, Wastara naye akamshikilia mume wake alipoandamwa na maradhi mpaka kifo kilipomchukua.

Mimi najua ni kiasi gani Wastara alihangaika kutafuta fedha za matibabu kwa ajili ya mume wake. Mapito waliyopita pamoja wengi yamewashinda. Tamaa za kibinadamu na matarajio ya muda mfupi, vikawafanya waachane wakati ambao mmoja anakuwa anahitaji msaada wa mwenzake.

Unamuacha mwenzi wako kisa anaumwa, auguzwe na nani? Ukichunguza kwa makini utaona kwamba kufanya hivyo siyo tu usaliti, bali ni ukatili wa kiwango kikubwa. Unaweza kumsababishia akafa kwa kihoro katika kipindi ambacho hakukitarajia.

Mpenzi wako amepata matatizo, yupo jela. Badala ya wewe kuonesha uaminifu wako ukawa unakwenda kumjulia hali na kumfariji amalize kifungo chake au aione mahabusu ni rahisi, huku ukimsaidia namna ya kushinda kesi, unamtelekeza bila huruma.

Utamu wa dunia kwa upande mmoja na majanga katika sehemu nyingine, ni kichocheo cha mapenzi kutetereka au kufa kabisa. Mwanamke anajionea jinsi ambavyo mwenzi wake anavyosota, hana fedha lakini mtaa wa tatu kuna mwanaume mwenye fedha zake anamtaka.

Mke anaumwa, mume anakutana na wanawake wa kila aina. Wengine ni rahisi kiasi kwamba hawangoji kutongozwa, wao wenyewe wanakuwa wa kwanza kurusha ndoano. Mwanaume anapovuka vishawishi hivyo na kuendelea kushikamana na mkewe, anakuwa ametimiza maana halisi ya mapenzi.

Sajuki na Wastara wanapata alama nyingi zaidi kwa sababu ya kigezo cha umri. Wamepata mitihani wakati ambao ni vijana wadogo, wazuri, maarufu na kadhalika. Walikuwa na sifa nyingi ambazo zingeweza kuwafanya washawishike kusalitiana.

Jumlisha na kawaida ya walimwengu kusemana. Ukioa au kuolewa watasubiri ndoa ivunjike ndiyo wakae pembeni wakucheke. Badala ya kukushauri au kukusaidia ndoa yako idumu, wao wanakuwa kama fisi anayesubiri mkono wa binadamu uanguke.

Hata ukipata kazi wao watasubiri ufukuzwe, ukianza biashara watangoja ianguke, ukipata cheo watatamani mambo yaharibike ili mradi wapate la kusema. Maneno yasiyo na msingi hayakuwa na nafasi ndani ya vichwa vya Wastara na Sajuki.

Hawakuvunjwa moyo wala kukatishwa tamaa na misukosuko iliyowakuta. Wakawa na mioyo ya chuma, wakasonga mbele bila kurudi nyuma. Ona sasa, leo tunaweza kuandika makala, kupongeza na kuwatumia kama mfano wa mapenzi ya kweli.

Kuna wale waliokuwa wepesi kuzusha. Ndani ya uhusiano wa Wastara na Sajuki, yakaibuliwa mambo ambayo kama si imani ya kila mmoja kwa mwenzake, basi wangeweza kukimbiana mapema. Hata uchawi ukanenwa.

Wapo waliothubutu kusema kwamba ili Sajuki apone ni sharti amwache Wastara. Binadamu wana mengi sana. Wao wakafumba macho, wakaweka pamba masikioni, wakayakabili yanayowahusu, ya walimwengu wakayaacha kwa ulimwengu.

Kama Winnie Mandela alimvuruga mzee Nelson Mandela, kwa nini usione kama Wastara ni mwanamke wa kipekee? Ikiwa mke wa Ayubu alichoshwa na mitihani ya mumewe alipopatwa na maradhi ya kila aina, mpaka akamkufuru Mungu kwa maneno, kwa nini usimsifu Wastara alipomvumilia Sajuki

Mungu ni sababu ya kila kitu. Juma Issa Kilowoko ‘Sajuki’ ameshatangulia mbele ya haki. Jambo zuri kwetu sisi ni kujifunza kwa yale aliyoyaacha kama mfano wa kuigwa. Yeye na mkewe, Wastara Juma Issa, wameonesha kitu kikubwa sana katika uhusiano wa kimapenzi

Wanaume waamue kupenda na kukubali mitihani ya namna yoyote itakayowakuta wapenzi wao. Wafanye kama alivyoweza Sajuki pale mwenzi wake Wastara alipopata ajali, akakatika mguu. Inawezekana tu kama unakuwa na moyo wa kweli.
Wanawake washike njia ya Wastara. Maradhi au matatizo ya aina yoyote watakayoyapata wapenzi wao, kwao iwe ni changamoto ya kulazimisha kuivuka. Kuna heshima na baraka nyingi katika kufanya kama alivyotenda Wastara kwa Sajuki.Vilevile, ieleweke kuwa kuna laana katika kumkimbia mwenzi wako pale anapopatwa na matatizo. Hayakuumbwa majanga bila ya kuwepo kwa binadamu. Unaweza kumkimbia mpenzi wako kisa kapata ajali na kutokwa meno, wiki inayofuata nawe yakafika, ukawa chongo.
Mwenzi baadaye anaweka meno ya bandia, anaweza kusimama mbele za watu na kutabasamu, wewe inakuwa ngumu, kwani jicho ndiyo hilo limekwenda zake. Kila mtu akiutakasa moyo wake na akapenda kikwelikweli, mapenzi yatakuwa rahisi mno.

Ni somo tu, watu wajionee maisha jinsi yalivyo. Wakati Wastara anamvumilia Sajuki pamoja na mitihani mikubwa waliyokuwa nayo, wapo wanawake wanaopata kila wanachohitaji, fedha zipo lakini wanasaliti ndoa zao mchana kweupe.
Jiulize wewe ndugu yangu, ni heshima gani ambayo Wastara anapewa leo hii? Kama angemfanyia Sajuki kinyume chake, kwa hakika hivi sasa angekuwa anasemwa vibaya sana. Kinyume cha heshima ni dharau. Nawe unaweza kuamua leo kwamba uheshimiwe au udharauliwe.
Mtu anaweza kudhani kwamba Wastara alimkuta Sajuki akiwa na maisha mazuri pamoja na umaarufu wake. La hasha! Walikutana wakiwa wadogo lakini wakaunganisha ndoto na matarajio ya kufanikiwa pamoja. Malengo yao yalikuwa ya dhati ndiyo maana mwisho wao ukawa huo.
Waliposema “kifo kitutenganishe”, walimaanisha kweli. Mitihani haikuwatenganisha mpaka Sajuki akatangulia mbele ya haki, Wastara akamzika, na sasa anakaa eda. Hicho ni kipimo thabiti kuwa waliamua kupendana kiukweliukweli. Ingekuwa wanafanya utani, wangeachana siku nyingi zilizopita.

Kuuguza ni mtihani mzito hasa pale inapotokea kwamba mgonjwa mwenyewe anakuwa ameugua kwa muda mrefu. Zipo changamoto ambazo hujitokeza ndani, hususan pale mgonjwa mwenyewe anapoathirika kisaikolojia.
Wapo ambao waliwasusa wagonjwa wao kwa sababu ya kuchoka maneno. Unaweza kufanya kile ambacho unakiona wewe ni kizuri lakini mwenyewe akahisi unamnyanyapaa. Wastara na Sajuki walikuwa marafiki mpaka Mungu alipotekeleza wito wake kwamba kila nafsi itaonja mauti.

Mshikamano ambao waliuonesha ni urithi mkubwa hata kwa mtoto wao ambaye Sajuki amemuacha akiwa mdogo sana. Akikua, atapata simulizi ya namna ambavyo wazazi wake walishikamana kwa upendo katika vipindi vyote vya matatizo mpaka kifo kilipowatenganisha.
Atawaona wazazi wake ni mashujaa kweli. Ni ukweli kuwa kama Sajuki angemsaliti Wastara alipopata ajali na kukatika mguu, vilevile mtoto huyo asingezaliwa. Ina maana kwamba upendo na mshikamano wao, vilisababisha mtoto Fahreen akazaliwa.

Tujifunze sasa, Mungu huwa haiachi mitihani ije tu, bali huwa na maana yake. Unatakiwa kushikamana na mwenzi wako kwa hali na mali. Zipo sababu ambazo zinaweza kuwafanya muachane lakini isiwe matatizo. Kumuona mwenzi wako hakufai kisa hana fedha ni ujinga sana.
Wewe mwanaume, umeona jinsi Sajuki alivyopewa taji la heshima kwa namna alivyohusika kimapenzi kwa Wastara. Wewe mwanamke, umejionea uvumilivu wa Wastara wakati wa matatizo ya Sajuki, basi sasa, wao wawe ni mfano kwako, pale unapohitaji kuona picha ya maana halisi ya mapenzi.

GLP

No comments: