TAARIFA KUTOKA TFF LEO
TAIFA STARS KUIVAA INTAMBA MU RUGAMBA APRILI 26
Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi
(Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya
miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu
mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji
waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.
Baadaye
wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji
wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa
Burundi.
Mechi
hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi
wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka
nchini Kenya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu
ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano
ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana
kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.
Hadi
muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao
2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti
tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Kwa
matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya
Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa
tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6
mwaka huu).
Timu
nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka
huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.
Katika
mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika
Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines
mabao 2-0.
No comments:
Post a Comment