Wednesday, March 5, 2014

BABA ACHARUKA, ASITISHA HARUSI YA BINTIYE ASIOLEWE NA MCHUNGAJI HUKO KENYA
Jeff Wanjau na Alice Mukami
KULIZUKA kioja katika kanisa moja mjini Othaya, Jimbo la Nyeri, mzee aliposimamisha harusi ya binti yake aliyepanga kuolewa na mpenzi wake ambaye ni kasisi.

Mzee Peter King’ori alisimama harusi ilipokuwa ikiendelea katika kanisa la Prophetic House of Mercy na kusema hangekubali binti yake aolewe na pasta huyo

Bw Kingori alihutubia waliohudhuria harusi hiyo akisema hangeruhusu binti yake, Alice Mukami, aolewe na Kasisi Jeff Wanjau kwa kuwa alikuwa ameoa mke mwingine kisha akamuacha.

Alisema alifahamishwa kuhusu harusi hiyo mnamo Ijumaa mwendo wa Saa Nne asubuhi na akakasirika kusikia binti yake alipanga kuolewa na pasta huyo.

“Huyu bwana harusi mnayemuona hapa alikuwa ameoa  mwanamke mwingine na akamuacha  na siwezi kukukabali binti yangu aolewe na mtu ambaye kazi yake ni kuoa wanawake kisha kuwaacha,” akasema Bw Kingori.

Aliongeza kwamba kama angefahamu kuhusu mipango ya harusi mapema angeenda mahakamani kupata agizo la kusimamisha wawili hao kuoana.

Ghafla tu baada ya hotuba yake hiyo, Kasisi Wanjau na Bi Mukami walitoroka wakitumia gari walilokodisha.

Akiongea na wanahabari baadaye, Wanjau alikanusha madai ya mkwe wake akisema alikuwa amemfahamisha kwamba alitaka kumuoa binti yake lakini akakataa.

Hata hivyo alikiri kuwa alikuwa ameoa mke mwingine na wakazaa watoto wawili lakini wakatalikiana baada ya kutofautiana.

Kasisi huyo alisema ingawa harusi ilitibuka ataendelea kuishi na Bi Mukami kama mtu na mkewe.

“Sioni sababu yoyote ya kukosa kumuoa Bi Mukami kwa sababu nina cheti cha talaka kwa mke wangu wa kwanza na sasa niko huru kuoa mwanamke yeyote ninayemtaka,” akasema.

Aliongeza kuwa harusi yao ilikuwa imekubaliwa na askofu wa kanisa lake ambaye alitangaza kwamba Wanjau alitalikiana na mkewe na akampa idhini ya kuoa mke mwingine. Kwa upande wake, Bi Mukami alisema haoni shida yoyote ya kuolewa na Kasisi Wanjau kwa kuwa anampenda sana na hawezi kumuacha.

“Ninampenda sana na sitamuacha hata kama wazazi wangu wanapinga harusi yetu. Tutaendelea kuishi pamoja kwa sababu tumekubaliwa na kanisa letu,” akasema Bi Mukami.

Hata hivyo, Kasisi Wanjau alisema yuko tayari kupatana na wakwe wakati wowote ule hata kama atakuwa amemuoa binti yao.

Kusimamishwa kwa harusi hiyo kulisababisha hasara kubwa  huku chakula kilichotayarishwa kikiharibika.

Umati mkubwa wa watu waliofika kanisa kushuhudia walitawanyika na kwenda zao baada ya harusi kutibuka.

No comments: