MWANAMKE AMDANGANYA MUMEWE KWAMBA AMETEKWA NYARA,
AKUTWA AKIPONDA RAHA NA HAWARA
![]() |
Bi Mary Njeri, wakati akiwa kituo cha polisi cha Karatina |
POLISI
wa Karatina, eneo la Nyeri nchini Kenya, wanamzuilia mwanamke aliyepatikana
akiponda raha siku mbili baada ya kujifanya alitekwa nyara kwa lengo la
kumlaghai mumewe Sh500,000.
Bi
Mary Njeri, mwenye umri wa miaka 22, alipatikana katika nyumba moja ya wageni eneo
la Thogoto, Kiambu, mnamo Jumapili mchana akiwa na mwanamume mwingine, baada ya
kudai alitekwa nyara na watu wasiojulikana akielekea Karatina kutoka nyumbani
kwake, eneo la Ngandu, Nyeri, Ijumaa iliyopita.
Polisi
walisema Njeri alidai alitekwa nyara na wanawake wawili na mwanamume mmoja na
wakamlazimisha kupanda gari walilokuwa nalo aina ya Probox.
Afisa
mkuu wa polisi Karatina (OCPD), Bw Rashid Mohammed, alisema alipata habari za
kutekwa nyara kwa mwanamke huyo Ijumaa jioni na akatuma maafisa wake mara moja
kumtafuta katika maeneo waliyoshuku alizuiliwa.
“Kufuatia
msururu wa visa vya utekaji nyara katika eneo la Kirinyaga, hatukutaka kuharibu
dakika hata moja. Mimi binafsi niliongoza shughuli za kumwokoa na nikatuma
maafisa wangu maeneo tuliyodhani angepatikana,” akasema Bw Mohamed.
Mume
wa mwanamke huyo, Bw Peter Kabingu, ambaye ni dereva wa matatu (daldala), alisema mpwa wake
alimpigia simu kumjulisha kuwa mkewe alitekwa nyara akielekea Karatina.
Alisema
siku hiyo mkewe alikuwa amepanga kukutana na mpwa wake huyo ili wamsaidie dada
yake kujiandaa kwa harusi.
“Tulikubaliana
aje mjini (Karatina) adhuhuri kukutana na mpwa wangu ili wampeleke dada yangu
kwa fundi kupima nguo ya harusi,” akaeleza Bw Kabingu.
Lakini
mwendo wa Saa Kumi na Moja jioni mpwa wake alipokea ujumbe kutoka kwa Njeri
akimwambia alitekwa nyara na kuwa yeye watekaji wake walikuwa wakielekea
Kirinyaga.
“Nilijaribu
kumpigia simu lakini ilikuwa imezimwa, nikajua mambo hayakuwa sawa,” akasema Bw
Kabingu.
Anasema
alitafuta msaada wa mwakilishi wa wadi yao ambaye alipiga ripoti katika kituo
cha polisi cha Karatina na shughuli za kumtafuta mkewe zikaanza.
“Sikulala
Ijumaa usiku nikiwaza kuhusu yaliyompata mke wangu ambaye tumeishi pamoja kwa
miaka minne sasa. Nililazimika kumtunza mtoto wetu mdogo,” akaeleza Bw Kabingu.
Jumamosi
asubuhi, alipokea simu kutoka kwa waliodaiwa kuwa watekaji nyara wakitaka fidia
ya Sh500, 000 ili wasimuue mkewe.
Baada
ya kujadiliana, watekaji nyara hao walimtaka awatumie Sh10,000 kwanza ili
waweze kuwasiliana naye. Alisema alisaidiwa na marafiki kupata pesa hizo na
akazituma kupitia nambari ya simu ya mkewe kisha akaanza kutafuta zilizobaki.
Wakati
huo polisi walikuwa wakiendelea kumsaka mkewe na Jumapili asubuhi wakampata
eneo la Thogoto Kaunti ya Kiambu akiwa na mpenzi wake, Peter Mugo.
Bw
Kabingu alisema hakuamini alipoambiwa mkewe alipatikana akiponda raha na
mwanamume mwingine kwa kutumia pesa alizokusanya kwa shida ili kumwokoa.
“Nimefanya
niwezalo kumfurahisha. Nimekuwa nikimtimizia mahitaji yote na hatujawahi
kukosana kwa miaka minne ya ndoa yetu. Sielewi ni kwa nini alinifanyia haya,”
akasema Bw Kabingu huku akitokwa na machozi.
Alisema
ataamua hatua ya kuchukua baada ya kushauriana na wazazi na wakwe wake.
No comments:
Post a Comment