TAARIFA YA
MAKABIDHIANO YA OFISI YA TFF YALIYOFANYIKA KATIKA OFISI ZA TFF JIJINI DAR ES
SALAAM TAREHE 2 NOVEMBA 2013
![]() |
Malinzi akizungumza na Tenga wakati akienda kumuachia ofisi |
Mheshimiwa Rais wa
TFF,
Pongezi na
Shukurani
1.
Naomba nianze kwa kushukuru kwa kukubali kufanyika kwa shughuli hii ya
makabidhiano ya Ofisi. Utaratibu huu haupo kikatiba wala katika kanuni zetu,
lakini ni muhimu sana kwa vile unatoa taswira ya uongozi endelevu na
ushirikiano unaostahili kuwepo baina ya uongozi mpya na ule wa zamani.
2.
Aidha napenda, kwa mara nyingine, kukupongeza kwa dhati wewe binafsi kwa
kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Shirikisho letu pamoja na kumpongeza Makamu wa
Rais na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa ushindi wao.
3.
Tumeshuhudia mchakato wa uchaguzi uliofanyika kwa uwazi, na ulio huru na wa
haki. Ninawashuru sana na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati ya Uchanguzi kwa ueledi
na kazi nzuri walioifanya. Kwa kiwango hicho hicho ninawapongeza na kuwashukuru
Wajumbe wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wa Kamati za Maadili – ngazi ya
awali na ya rufani – kwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na vyema.
4.
Nawajibika kutoa pongezi kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kukamilisha kazi
muhimu ya kutuchagulia viongozi wetu kwa utulivu mkubwa.
5.
Utulivu wakati wa mchakato mzima wa
uchaguzi – kuanzia mwanzo hadi mwisho – ni kielelezo cha ukomavu wa uongozi wa
mchezo wa mpira wa miguu nchini. Natoa shukurani za dhati kwa wanachama na
wadau wote wa mpira wa miguu nchini kwa mchango wao wa hali na mali katika
kufanikisha zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa mpira wa miguu nchini.
Dir a na Malengo ya
Uongozi Uliopita
6.
Dira ya uongozi uliopita ilikuwa ni kujenga mazingira mazuri na endelevu ya
maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini. Hii ilitokana na hali ya migogoro
isiyoisha na malumbano ya mara kwa mara yaliyokuwepo kabla ya kuingia
madarakani.
7.
Ili kufanikisha dira yetu, uongozi
uliopita ulidhamiria kujenga msingi bora wa uongozi wa mpira wa miguu nchini,
hivyo kujiwekea malengo yafuatayo:
·
Kutengeneza Katiba mpya na Kanuni zitakazokidhi mahitaji ya nchi yetu ya
kudumisha demokrasia na utawala bora – uwazi, uwajibikaji, na kadhalika.
·
Kuhakikisha kuwa Katiba yetu na Kanuni zetu zinazingatiwa na kuheshimiwa.
·
Kuweka Kanuni za Fedha na kuchukua hatua za kujenga uaminifu katika usimamizi
wa ukusanyaji, utunzaji na matumizi ya fedha. Tuliazimia kuona hesabu za
Shirikisho zinakaguliwa na wakaguzi wenye sifa za kimataifa, na taarifa ya
ukaguzi kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu kila mwaka, bila ya kukosa.
·
Kuwa na mfumo wa mashindano utakaongeza ushindani na kuchochea uwekezaji. Azma
ilikuwa ni kuongeza idadi ya mashindano ili kutoa fursa kwa vipaji kuonekana na
kuendelezwa.
·
Kuweka jitihada katika mafunzo ya wataalamu wa mpira wa miguu nchini kwa
kuongeza idadi na kozi/semina za mafunzo ya uongozi, uamuzi, ualimu na udaktari
wa michezo.
·
Kujenga mfumo mpya wa uongozi wa timu za taifa. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha
kuwa timu za taifa zinakuwa na uongozi wake chini ya Mwalimu/Walimu wa timu ya
taifa na kuzitofautisha na Idara ya Ufundi, pamoja na kuhakikisha timu zetu za
taifa zinashiriki michezo mingi iwezekanavyo ya mashindano na ya kirafiki.
·
Kujenga uhusiano mzuri na wadau na washirika wetu, hususan wadau wetu wakuu
ambao ni Serikali na vyombo zake; Mashirikisho ya mpira tuliyojumuika nayo -
FIFA, CAF, na CECAFA; Wadhimini na Wafadhili wetu – kampuni, mashirikia ya umma
na watu binafsi - wanaochangia maendeleo ya mpira wa miguu nchini kwa hali na
mali.
·
Kuwa karibu na jamii na kuisaidia jamii. Nia ni kutumia umaarufu wa mchezo wa
mpira wa miguu nchini kuhamasisha maendeleo ya jamii, hasa katika masuala ya
afya ya jamii – kampeni ya malaria, ukimwi, kupambana na madawa ya kulevya na
kadhalika. Rais anayeondoka madarakani ni Balozi wa Malaria nchini na Rais wetu
mpya ni mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Malaria, chini ya Uenyekiti
wa Waziri wetu wa Afya, Mheshimiwa Hussein Mwinyi.
8.
Utekelezaji wa Dira tuliyojiwekea na malengo yetu ulifanyika kwa ushirikiano wa
karibu na wanachama na wadau wetu. Yaliyofanyika yanajulikana. Itoshe kusema
kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa jitihada kubwa na uadilifu mkubwa na kwamba
malengo tuliyojiwekea yalifikiwa.
9.
Katika hotuba niliyoitoa katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu uliopita – Jumamosi,
tarehe 26 Oktoba 2013, niliainisha kwa kina nini kilifanyika katika kipindi cha
uongozi uliopita pamoja na mafanikio ya kazi iliyofanyika. Napenda
kuimbatanisha hotuba hiyo kama sehemu ya taarifa hii ya makabidhiano.
10.
Matarajio yetu ni kuwa, baada ya jitihada za kuweka msingi wa uongozi na wa
maendeleo ya mpira wa miguu nchini, nguvu itaelekezwa katika kukuza kiwango cha
mpira wa miguu nchini mwetu. Tulichokifanya ni kutayarisha Mpango wa Muda
Mrefu wa Maendeleo ya Mpira Miguu Nchini – 2013 hadi 2016 (Long Term Technical
Development Plan – 2013 to 2016), ambayo umeambatanishwa kama sehemu ya
taarifa hii ya makabidhiano.
11.
Hivyo basi, uongozi mpya una kazi ya kusimamia na kufanikisha utekelezaji wa
Mpango huo. Pia, ni matarajio yetu kuwa uongozi mpya utayadumisha mambo ya
msingi tuliyojiwekea na kuufanyia kazi upungufu uliopo.
Shukurani kwa
Wanachama na Wadau wa TFF
12.
Pamoja na kuwa nimeshatoa shukurani mara kadhaa,
napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru wote waliotusaidia kufika hapa
tulipo. Nawashukuru sana wanachama wetu, wadau wetu wote – Serikali yetu na
vyombo vyake vyote, wadhamini na wafadhili, waandishi na vyombo vya habari,
wapenzi wa mpira na wananchi kwa ujumla kwa mchango wao wa hali na mali. Bila
yao tusingefika hapa tulipofika.
13.
Shukurani maalum zimwendee Mheshimiwa Rais wetu,
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa mchango wake usiopimika. Alikuwa ni sehemu
mabadiliko haya tangu mwanzo, hata kabla ya uongozi wetu kuingia
madarakani. Ametusaidia kwa kiasi kikubwa kuzijenga timu zetu za taifa
siyo tu kwa uamuzi wake wa kulipia mishahara ya walimu wa timu ya taifa, bali
pia kwa kuwahamasisha vijana wetu kwa hali na mali wafanye vizuri. Sina hakika
kuwa yupo Rais mwingine, popote pale duniani, aliye karibu na mapenzi ya dhati
kwa vijana wa timu zake za taifa zaidi ya Rais wetu. Zaidi ya hayo, Mheshimiwa
Rais amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utawala bora katika mpira wa
miguu nchini na amefanya kila aliloliweza kuona kuwa kiwango cha mchezo
kinapanda na timu zetu zinafanya vizuri. Napenda kutoa shukurani za dhati kwake
kwa uongozi na msaada wake.
Wanachama, Katiba
na Kanuni, Wafanyakazi, Mali na Mikataba ya TFF
14.
Wanachama
TFF ina jumla ya
Wanachama 44 ambao wote ni wanachama hai kama ifuatavyo:
·
Vyama vya Mikoa – 25
·
Vyama Shiriki
- 5
·
Vilabu vya Ligi Kuu - 14
15.
Katiba na Kanuni
Hivi sasa TFF ina
Katiba Mpya (ya Mwaka 2013) iliyofanyiwa marekebisho ya mwisho na Mkutano Mkuu
Maalum wa TFF tarehe 13 Julai 2013.
Pamoja na Katiba
TFF ina kanuni zifuatazo ambazo kwa mujibu wa Katiba ya TFF hupitishwa na
kamati ya Utendaji:
·
Kanuni za Fedha
·
Kanuni za Mashindano kuanzia Ngazi ya Wilaya hadi Ligi Kuu
·
Kanuni za Utii
·
Kanuni za Nidhamu
·
Kanuni za Maadili
·
Kanuni za Uchaguzi za Uchaguzi za TFF na za Wanachama wa TFF
·
Kanuni zinazosimamia Uendeshwaji wa Bodi ya Ligi Kuu
·
Kanuni za Mashindano mengine, kama vile Copa Coca Cola, Uhai Cup, Super 8 na
Taifa Cup. Ni vyema ikafahamika kuwa kila mashindano lazima yawe na Kanuni
zinazosimamia uendeshwaji wake.
TFF inalazimika
kuzifanyia marekebisho Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wake kufuatia
marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za TFF. Aidha, TFF inadeni la kutayarisha
Kanuni za Chombo cha Usuluhishi (Arbitration Tribunal) kama ilivyoainishwa
katika Katiba. Hivi karibuni, TFF imepokea Kanuni za Mfano kutoka FIFA ambayo
ipo haja ya kazi hii kukamilishwa na uongozi mpya.
16.
Wafanyakazi wa TFF
Hivi sasa TFF ina
jumla ya wafanyakazi 29. Kati yao yupo/wapo
·
Katibu
Mkuu
- 1
·
Wakurugenzi / Maofisa
Mwandamizi
- 5
·
Wafanyakazi wengine
-
23
Katibu Mkuu na
Wakurugenzi wapo katika kipindi cha nyongeza cha miezi sita (6) cha mikataba
yao, kinachoishia mwishoni mwa mwezi Desemba 2013. Wafanyakazi wengine
wapo katika mikataba ya miaka minne yenye kipindi cha majaribio cha miezi sita
kuanzia mwanzoni mwa mwezi Septemba 2013. Hivyo basi, uongozi mpya una nafasi
ya kufanya tathmini ya mahitaji ya TFF kisha kufanya uamuzi juu ya ajira za
Wafanyakazi waliopo kadiri utakavyoona inafaa.
TFF ilichukua hatua
ya kuingia kufanya makubaliano ya hiari na wafanyakazi wake ili kuondokana na
ajira za maisha (Permanent Employment) na kubaki na ajira za mikataba (Contract
Empoyment) kwa wafanyakazi wake wote.
Wafanyakazi wa TFF
wamekuwa wakifanya kazi ngumu na saa nyingi kuliko kawaida. Ajira ya TFF haina
saa za ziada wala siku za mapumziko. Kutokana na dhana ya kujitolea na ukweli
kwamba shughuli nyingi za TFF, kama vile michezo na mikutano hufanyika siku za
mwisho wa wiki na sikukuu, ni dhahiri kuwa Wafanyakazi wa TFF wamekuwa
wakilazimika kufanya kazi siku hizo, na mara nyingi bila malipo ya saa za
ziada. Aidha, kutokana na kukosa uwezo, uongozi uliopita ulishindwa kupandisha
mishahara yao ipasavyo.
Napenda kuchukua
nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa kuihudumia TFF na mpira wa miguu
katika mazingira magumu sana. Tunauomba uongozi mpya uliangalie suala hili kwa
umakini, kama moja ya hatua za kuongeza ufanisi wa Sekretariati.
17.
Mali za TFF
Hivi sasa TFF ina mali zifuatazo:
·
Kiwanja cha Karume Stadium, chenye hati namba 27026 iliyotolewa tarehe 10
Novemba 1981. Kiwanja cha Karume kina ukubwa wa ekari 8.26. Ombi la kuingezea
muda hati hiyo limeshapelekwa na linafuatiliwa.
·
Ndani ya Kiwanja hicho, kuna Jengo la ofisi ya TFF, Jengo la Kituo cha Ufundi
(Technical Centre) na Uwanja wa nyasi za bandia wa Karume.
·
Kiwanja cha Tanga chenye ukubwa wa hekta 7.6 (ekari 19) kilichopo katika eneo
zuri sana mjini Tanga. Kiwanja hiki tayari kimeshalipiwa na hivi sasa taratibu
zinaendelea kukamilisha taratibu za kukiandikisha na kupata hati.
·
Magari sita (6) na Trekta moja (la kusafishia uwanja wa nyasi bandia). Magari
hayo ni: Bus kubwa aina ya Yutong, basi dogo aina ya Coaster, magari ya aina
4WD Ford Everest, Rav 4, Suzuki Escudo na Honda CVR. Mawili kati magari hayo -
Suzuki Escudo na Honda CVR – yanatumika lakini hayapo katika hali nzuri.
Ni vyema uongozi mpya ukayafanyia tathmini magari hayo na kufanya maamuzi
muafaka kadiri utakavyoona inafaa.
·
Fedha taslimu Shilingi 33,518,000 na US$ 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa.
Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya Mkutano
Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi 56,240,000
yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya Timu ya Taifa ya Wanawake U-20 na
gharama za mchezo baina ya timu yetu ya Taifa na ile ya Msumbiji uliofanyika
wiki iliyopita. Hata hivyo, leo hii US$ 415,000 (Shilingi 664,000,000)
kimehamishwa kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha
hizo zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki ijayo. Malipo
haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita lakini yalicheleweshwa
ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za udhamini wa TBL kufanyika.
Zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo yamefanyika.
Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya US$ 420,000 (Shilingi 672,000,000)
yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa - katikati ya mwezi huu wa
Novemba 2013.
Hivyo basi, uongozi
unaoingia madarakani hautaanza kwa shida. Ni matarajio yetu kuwa hatua ya awali
itakuwa kurejesha fedha kwenye akaunti zilikoazimwa kinachofikia US$ 166,509 -
US$ 148,174 kutoka kwenya Akaunti za FAP na US$ 18,335 kutoka kwenye Akaunti ya
TRA - kwa ajili ya kugharimia Mkutano Mkuu na matumizi ya Taifa Stars kwa ajili
ya matayarisho na safari ya kwenda Gambia.
Ili kujiridhisha
kuwa fedha za udhamini zinatumika kama ilivyokubalika katika mikataba, TFF
imetoa nafasi kwa wadhamini kufanya ukaguzi wa fedha inazozitoa wakati wowote
ule. Utamaduni huu tumekuwa nao katika kipindi chote cha utawala wa uongozi
wetu, ili kutoa imani kwa wadhamini na kuhakikisha kuwa malengo ya udhamini
husika yanafanikiwa. Huu ni utaratibu mzuri na ni matumaini yetu kuwa
utadumishwa.
Jengo la Kituo cha
Ufundi ndiyo kwa limekamilika kukarabatiwa na bado halijafunguliwa rasmi.
Ukarabati huo umefanikisha kutengenezwa kwa mfumo wa maji machafu
unaojitegemea. Hivyo, kutohitaji kutengemea mashimo ya Jengo la Ofisi za TFF.
Hatuo ya mwisho ya kazi hiyo ni kukamilisha ukaguzi wa matumizi yaliyofanyika
katika ukarabati huo na kuiwasilisha CAF mapema iwezekanavyo. Hayo ndiyo
makubaliana kuhusiana na msaada uliotolewa na CAF – unaojulikana kama CAF
FAP 2.
Ukarabati wa Kituo
cha Ufundi umefanywa, pamoja na sababu nyingine, ili kutoa fursa kwa Mradi wa
Ujenzi wa Karume kuendelea. Kama nilivyoeleza katika Mkutano Mkuu, dhamira ni
kuwekeza katika Mradi wa Ujenzi wa jengo / majengo yenye hadhi kubwa kwa ajili
ya kukodishwa kuzunguka uwanja huo. Jengo lililo karabatiwa na uwanja wa mpira
vitabaki na kuendelea kutumiwa kama Kituo cha Mafunzo. Jambo la muhimu ni
kuhakikisha kuwa uwekezaji katika mradi huo hauhitaji dhamana ya uwanja wetu na
majengo yetu. Ni imani yetu kuwa njia muafaka inapatikana, ikiwa ni pamoja na
utaratibu wa ‘Build, Operate and Transfer’ (BOT).
18.
Hesabu za TFF
Ripoti ya Ukaguzi
wa hesabu za TFF hadi kufikia Desemba 2012 iliwasilishwa katika Mkutano Mkuu
uliopita. TFF ilipata Hati Safi ya Ukaguzi wa hesabu zake na Mkutano Mkuu
ukaikubali na kuipitisha ripoti hiyo hesabu za mwaka 2012. Aidha, taarifa ya
hesabu za TFF kwa kipindi cha kuanzia tarehe 1 Januari hadi 30 Septemba 2013
kusambazwa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Ifahamike kuwa TFF
imekuwa ikipata Hati Safi, kila mwaka katika kipindi cha miaka minane
iliyopita. Hatuna shaka kuwa hali hii itaendelea.
19.
Mikataba ya Udhamini
TFF inayo mikataba ifuatayo ya udhamini na Wadhamini wafuatayo:
·
Vodacom – Udhamini wa Ligi Kuu
·
TBL – Taifa Stars
·
Coca Cola – Mashindano ya Copa Coca Cola
·
SSB & Co – Mashindano ya Uhai
·
Bank ABC – Super 8
·
Azam Media – Haki za Matangazo ya Television kwa Ligi Kuu
Aidha, baadhi ya
vilabu kama vile Yanga na Simba vinadhaminiwa na TBL, Coastal Union
inafadhiliwa na Tanga Cement na Azam FC inadhaminiwa na Azam Cola.
Changamoto
zinazoikabili TFF
20.
Zipo changamoto nyingi zinazoikabili TFF lakini
kubwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na ambazo uongozi mpya hauna
budi kuzishughulikia ni ulazima wa:
·
Kuendeleza sola la vijana na watoto kwa kutoa fursa kwa watoto/vijana wengi
kupata malezi mazuri ya uchezaji wa mpira wa miguu ili kupanua wigo wa kupata
wachezaji wenye vipaji. Katika jambo hili bado tuko nyuma sana. Tulididimia
sana kutokana na kufutwa kwa michezo mashuleni. Ipo haja ya uongozi mpya
kushirikiana na Serikali kuhamisha michezo shuleni, kama hatua ya wali ya
kutatua tatizo la soka la vijana/watoto.
·
Kuendeleza soka la wanawake. Matatizo ya soka la wanawake yanafanana na ya soka
la vijana. Tofauti ni ndogo sana. Kama ilivyo kwa soka la vijana, hatua muhimu
kufanyika kwa jitihada ya kuwahamasisha wasichana wacheze mpira wa miguu
shuleni.
·
Kuhakikisha ueledi unazingatiwa katika uongozi wa Vilabu na Vyama Wanachama wa
TFF. Kinyume chake hatutaweza kushindana na wenzetu ambao walishapiga hatua
katika taaluma ya uongozi wa michezo. Vilabu vyetu ni lazima vihakikishe
kuwa vinatimiza masharti ya ‘Club Licencing’ kama yalivyotolewa na CAF, pamoja
na marekebisho yake. Huu ni mtihani kwetu. Ni lazima tufaulu kutimiza masharti
hayo, vinginevyo tutabaki nyuma. Ipo haja ya kuuangalia kwa mfumo wa uongozi wa
Vilabu vyetu na Vyama Vyetu kwa azma ya kubuni mfumo utakaotuletea ufanisi
zaidi wa kiungozi na uendeshaji kuliko ilivyo hivi sasa.
·
Kuhamasisha uwekezaji katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu nchini.
Tuna upungufu mkubwa wa vifaa na viwanja vya kuchezea. Ni vigumu
kuundeleza mchezo wa mpira bila ya kuwa na viwanja vya kuchezea na vifaa.
Aidha, zinahitajika raslimali watu na fedha katika kulea na kuwaendeleza
wachezaji na wataalamu wetu. Licha ya hapo kiasi kikubwa cha fedha kinahitajika
kwa ajili ya matumizi mengine ili timu ifanye vizuri. Kwa maneno mengine
tunahitaji kufanya kila jitihada kuhamasisha watu binafsi, makampuni na Serikali
iwekeze katika mpira, wadhamini zaidi wajitokeze na wapenzi wengi zaidi
wachangie timu zao – kwa njia mbalimbali - ili kuongeza mapato ya vilabu na
vyama husika. Vilabu vyetu na Vyama Wanachama wa TFF vinakabiliwa na upungufu
mkubwa wa fedha za uendeshaji. Mawazo au fikra kuwa kuna fedha nyingi
katika mpira wa miguu ni dhana isiyo na msingi na inayotokana na kutofahamu
gharama za uendeshaji wa vilabu na vyama vyetu. Pamoja na ongezeko kubwa la
mapato ya milangoni na mchango wa udhamini katika kipindi cha uongozi uliopita,
bado kinachopatikana hakikidhi hata theluthi moja ya mahitaji muhimu. Haja ya
kuongeza mapato ndiyo changamoto mama. Ikitatuliwa itasaidia kwa kiasi kikubwa
kupunguza makali ya changamoto nyingine.
·
Ili kuvutia uwekezaji, udhamini na misaada kwenye mpira wa miguu, ni lazima
tuhakikishe kuwa tunaendelea na jitihada za kujenga uaminifu wa utunzaji na
matumizi ya fedha ndani ya TFF. Ipo haja ya kuhakikisha kuwa Kanuni za Fedha
zinazingatiwa na hesabu zetu zinakaguliwa mara kwa mara. Mpango wa Tiketi za
Elektroniki ni muhimu usimamiwe kwa nguvu zote kwa vile sio tu utatuongezea
mapato bali pia utatoa picha ya uaminifu na ueledi.
Uhusiano na ZFA
21.
TFF haina budi kufanya kila linalowezekana kudumisha uhusino mzuri baina yake
na ZFA. TFF inatambulika na FIFA kama msimamizi wa mchezo wa mpira wa miguu
nchini Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa mchezo wa mpira katika visiwa vya Unguja
na Pemba unasimamiwa na ZFA. Hakuna matarajio ya hali hiyo kubadilika. Kwa
sababu hiyo, upo ulazima wa kudumisha uhusiano uliopo na kuhakikisha kuwa ZFA
inapata haki ya kupewa baadhi ya miradi inayotokana na fedha za FIFA – FAP. Kwa
vile fedha hizo hatolewa kwa njia ya miradi, utaratibu tuliokubaliana ni
kuhakikisha kuwa kila mwaka baadhi ya miradi / semina zinafanyika visiwani.
Wakaguzi wa Hesabu
za TFF
22.
Hesabu za TFF zinakaguliwa makampuni ya Ukaguzi wa Hesabu yafuatayo:
·
TAC Associates – kwa hesabu zote za TFF
·
KPMG – kwa fedha za FIFA
Bodi ya Wadhamini
23.
Mkutano Mkuu wa Mwaka 2011 uliridhia kuundwa kwa
Bodi ya Wadhamini wa TFF na Mkutano Mkuu uliopita ulipitisha majina ya Wajumbe
wa Bodi ya Udhamini kama ifuatavyo:
·
Said El Maamry
– Mwenyekiti
·
Mh. Joel Bendera
– Makamu Mwenyekiti
·
Dr. Ramadhani Dau
–
Mjumbe
·
Steven Mashishanga
– Mjumbe
·
Mohamed Abdulaziz
- Mjumbe
Mheshimiwa Rais,
napenda kukubidhi taarifa hii ya makabidhiano leo hii tarehe 2 Novemba 2013 kwa
ufahamu na kumbukumbu za TFF. Tafadhali jisikie huru kuomba ufafanuzi wa jambo
lolote lililomo katika taarifa hii au kuomba taarifa juu ya jambo ambalo kwa
bahati mbaya limesahauliwa. Sekretariati ya TFF inawajibika kutoa
ufafanuzi unaohitajika.
Tunakutakia wewe
mwenyewe na uongozi wako kila la heri na mafanikio katika kuingoza wa TFF
kuelekea kule kunakotarajiwa na wapenzi wa mpira wa miguu nchini. Wadau na
wapenzi wote wa mpira wa miguu wanaoitakia heri nchi yetu wapo nyuma yako.
Leodegar
Tenga
RAIS WA
TFF
Angetile Osiah
KATIBU MKUU WA TF
No comments:
Post a Comment